Baraza la Makanisa Duniani laitaka Marekani iiondolee Iran vikwazo
Baraza la Makanisa Duniani na Jumuiya ya Kitaifa ya Makanisa ya Kristo zimeeleza wasiwasi wao juu ya athari mbaya za vikwazo vya Marekani dhidi ya wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Taasisi hizo za kidini zimeonyesha kusikitishwa na vikwazo hivyo vya kidhalimu vya Washington dhidi ya taifa la Iran, katika barua ziliyomuandikia Ebrahim Abuzar Torkaman, Mkuu wa Shirika la Uhusiano na Utamaduni wa Kiislamu (ICRO).
Katika barua hiyo, taasisi hizo za kidini zimemuasa Rais Donald Trump wa Marekani aiondolee vikwazo Iran katika mazingira ya sasa ya kukabiliana na janga la Corona, ili taifa hili liweze kudhamini mahitaji yake ya dawa, zana za tiba na chakula kupitia masoko ya kimataifa.
Sehemu ya barua hiyo ya Baraza la Makanisa Duniani na Jumuiya ya Kitaifa ya Makanisa ya Kristo inasema: Kwa mnasaba huu wa Pasaka, moja ya siku muhimu zaidi katika kalenda ya Wakristo kote duniani, na huku Waislamu wakijongewa na mwezi mtukufu wa Ramadhani, dunia inakabiliwa na changamoto mpya inayohitaji ushirikiano.
Barua hiyo imesisitiza kuwa, "katika moyo wa kuonyesha mshikamano wa kimataifa, na kwa kuheshimu misingi ya ubinadamu, na pia kufuatia mwito wa Umoja wa Mataifa wa usitishaji vita na uhasama katika kipindi hiki, tunakuomba (Trump) uiondolee Iran vikwazo vya kulemaza, vikawamo vikwazo vya kifedha, ili (Iran) iweze kupiga jeki jitihada zake za kupamba na virusi hivi angamizi."
Wiki iliyopita pia, kundi la wanadiplomasia na mawaziri wa zamani wa baadhi ya nchi walimuandikia barua Trump wakimtaka aiondolee Iran baadhi ya vikwazo hasa wakati huu wa mlipuko wa virusi vya Corona.
Kadhalika shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesisitiza kwamba, vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran vinapaswa kupunguzwa katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 ili nchi hii iweze kudhamini mahitaji ya dharura.