Marekani yawaliwaza kwa medali askari wake waliojeruhiwa katika shambulizi la Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i60788-marekani_yawaliwaza_kwa_medali_askari_wake_waliojeruhiwa_katika_shambulizi_la_iran
Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani imewatunuku medali za heshima makumi ya askari wake waliojeruhiwa katika shambulizi kali la Iran la mapema mwaka huu nchini Iraq.
(last modified 2026-02-17T02:26:49+00:00 )
May 05, 2020 08:04 UTC
  • Marekani yawaliwaza kwa medali askari wake waliojeruhiwa katika shambulizi la Iran

Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani imewatunuku medali za heshima makumi ya askari wake waliojeruhiwa katika shambulizi kali la Iran la mapema mwaka huu nchini Iraq.

Kapteni wa Jeshi la Majini la Marekani, Bill Urban amesema tayari askari watatu wamekabidhiwa medali hiyo ya 'Purple Hearts' baada ya kuidhinishwa na Luteni Jenerali Pat White, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Marekani nchini Iraq; huku wengine 23 wakitazamiwa kutunukiwa medali hizo baadaye wiki hii. 

Takwimu rasmi za Wizara ya Ulinzi ya Marekani zinaonyesha kuwa, wanajeshi 110 wa US walijeruhiwa katika shambulizi hilo la Januari mwaka huu 2020.

Itakumbukwa kuwa, Jumatano ya tarehe 8 Januari mwaka huu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilishambulia kambi kubwa zaidi ya wanajeshi wa Marekani nchini Iraq ya Ainul Asad, ikiwa ni katika kulipiza kisasi cha mauaji ya kigaidi yaliyofanywa na wanajeshi wa nchi hiyo dhidi ya aliyekuwa Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani na wanajihadi wenzake.

Baadhi ya askari wa jeshi vamizi la Marekani waliojeruhiwa Iraq

Awali Rais Donald Trump alidai kwamba, shambulizi hilo la makombora ya balestiki la Iran halikuwasababishia majeraha askari hao vamizi wa Marekani nchini Iraq, lakini baadaye Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo (Pentagon) hatua kwa hatua ilianza kutangaza idadi ya majeruhi wa kipigo hicho. 

Aidha wiki moja baada ya shambulizi hilo, gazeti la Washington Post lilifichua kwamba, wanajeshi wawili waliuawa kwa kurushwa kutoka kwenye mnara wa kambi hiyo na kwamba makumi ya wengine walipata majeraha mabaya ya kimwili na kiakili.