May 27, 2020 03:58 UTC
  • Joseph Borrell akiri kumalizika zama za uongozi wa Marekani duniani

Kuingia madarakani Rais Donald Trump wa Marekani huko White House mnamo tarehe 20 Januari 2017 kulifungua ukurasa mpya wa siasa za upande mmoja za nchi hiyo duniani.

Kupitia nara ya 'Marekani Kwanza', Trump aliweka maslahi ya nchi yake mbele ya kila jambo na bila kujali maslahi ya mataifa mengine akawa anadai kwamba  siasa za mabavu na kimaslahi ndizo zingeweza kudhamini nguvu na kuifanya Marekani kuwa kiongozi imara wa dunia. Pamoja na hayo lakini leo madai hayo yanatathminiwa kwa shaka kubwa.

Katika uwanja huo, Josep Borrell, Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya akizungumza siku ya Jumatatu alisema kuwa zama za udhibiti na uongozi wa Marekani duniani zinaelekea ukingoni na kutaka stratejia imara zichukuliwe kuhusu China. Alisema: Kwa muda mrefu, wataalamu wa mambo wamekuwa wakizungumzia kukaribia kumalizika zama za mfumo wa dunia ulio chini ya udhibiti wa Marekani na kuingia karne ya Asia. Kudhoofika na kumalizika nguvu za Marekani kulitabiriwa miaka mingi iliyopita na sasa kufuatia kuenea virusi vya corona mwenendo huo wa kudhoofika nguvu za Marekani unatimia kwa kasi kubwa zaidi.

Ukweli wa mambo ni kwamba kuenea virusi vya corona kumeleta mabadiliko makubwa ulimwenguni na kuisababishia Marekani matatizo makubwa ya kiuchumi, kijamii na kiafya. Kwa kuzingatia ukweli huo, viongozi wa siasa za nje wa Umoja wa Ulaya wanakuchukulia  kuenea kwa virusi vya COVID-19 kuwa nukta muhimu ya kubadilika uwiano wa nguvu kutoka nchi za Magharibi kuelekea Mashariki na sasa wanakiri kwamba wanapata mashinikizo makubwa ya kuchagua ni upande gani wa historia wanapasa kusimama.

Josep Borrell, Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya

Sula muhimu hapa ni kwamba akiwa kiongozi wa ngazi ya juu wa sisa za nje za Umoja wa Ulaya, Borrell anakiri ukweli ambao washindani na wapinzani wa Marekani wamekuwa wakiuzungumzia na kuusisitiza kwa miaka mingi katika ngazi za kimataifa. Ukweli huo si mwingine bali ni wa kudhoofika nguvu ya Marekani, jambo ambalo lina taarhira kubwa ndani na nje ya nchi hiyo. Kimataifa, Trump amevuruga na kuharibu nyenzo zote za ushirikiano wa kimataifa na kutekekeleza kwa nguvu zake zote, siasa za upande mmoja na za mabavu kwa lengo la kufikia malengo yake ya kimaslahi, jambo ambalo bila shaka limepunguza ushawishi na itibari yake mbele ya mataifa mengine ya dunia. Kwa maneno mengine ni kwamba kutokana na siasa zake hizo za mabavu, Trump amepelekea Marekani kupoteza ushawishi na nguvu yake laini katika ngazi za kimataifa na hivyo kutengwa na mataifa mengine.

Kwa kuitoa Marekani katika mikataba muhimu ya kimataifa, Trump amethibitisha kivitendo kwamba haipi umuhimu wowote misingi ya ushirikiano na mitazamo ya mataifa mengine na kwamba la muhimu kwake ni kuheshimiwa, kutiiwa na kudhaminiwa na wote maslahi ya Marekani. Rais huyo mwenye utata wa Marekani alianza kwa kuiondoa Marekani katika mkataba wa mazingira na hali ya hewa wa Paris na kisha mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) mwezi Mei 2018. Aliweka katika ajenda ya serikali yake juhudi za kuiondoa Marekani katika mkataba wa kudhibiti silaha za nyuklia na tayari ameitoa nchi hiyo katika mkataba wa silaha za masafa mafupi za nyuklia INF (Intermediate-Range Nuclear Forces Treaty) na pia Mkataba wa Mbingu zilizo Wazi (Open Skies Treaty) uliotiwa saini tarehe 24 Machi 1992 na hivi sasa inapanga kutourefusha mkataba wa START (Strategic Arms Reduction Treaty).

Trump akipingana hadharani na Rais Macron wa Ufaransa

Trump pia tayari ameiondoa Marekani katika Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) na vile vile Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo. Wakati huo huo Trump ni msababishaji mkuu wa vita vya kibiashara kati ya Marekani na China na pia na Umoja wa Ulaya. Nafasi ya nchi hiyo katika shirika la kujihamila NATO pia inatiliwa shaka kubwa. Siasa hizo za mabavu za Trump zimeleta mgawanyiko mkubwa kati ya Marekani na Ulaya kuhusiana na masuala mengi ya pande mbili za bahari ya Atlantic. Kwa mujibu wa Jean-Yves Ludrian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Trump aliingia Ikulu ya White House kwa nara ya 'Marekani Kwanza' lakini sasa hivi ameuweka mguu wake nje ya mipaka ya Marekani kwa kupiga nara ya 'Marekani Pekee.' Kupitia nara hiyo Marekani ambayo inavutana na nchi nyingine za dunia kwa lengo la kuhodhi madaraka na nguvu, daima hutaka kuwa mshindi katika kila mazungumzo na upande wa pili.

Katika hali hiyo washindani wawili wakuu wa Marekani mmoja akiwa katika uwanja wa kisiasa na kijeshi yaani Russia na mwingine katika uwanja wa biashara na uchumi yaani China, zinakosoa vikali mitazamo na siasa za Trump katika ngazi za kimataifa. Siasa za upande mmoja za Marekani mbazo zimeipelekea kudhani kuwa ndiyo nguvu kubwa ya pekee duniani na hivyo kuyaainishia taklifu mataifa mengine kwa msingi wa dhana hiyo potovu, ni moja ya ukosoaji mkubwa wa Russia dhidi ya Marekani. China pia inaamini kuwa siasa hizo za upande mmoja za Trump zimeibua vita vya biashara kati yake na Marekani na pia na mataifa mengine ya ulimwengu na hivyo kupunguza ustawi wa uchumi na kuzidisha mataizo ya kiuchumi katika nchi tofauti za dunia.

Tags