Jun 08, 2020 12:22 UTC
  • Russia: Washington itekeleze kivitendo maagizo yake kuhusu haki za binadamu

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imeitaka Washington itekeleze kivitendo maagizo yake inayoyatoa kuhusu haki za binadamu. Russia imeyasema hayo ikiwa ni radiamali yake kwa siasa zinazotekelezwa na serikali ya Marekani katika kuyakandamiza vikali maandamano ya wananchi dhidi ya ubaguzi wa rangi wanaofanyiwa wananchi wa nchi hiyo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia leo imetoa taarifa ikiashiria maandamano makubwa dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Marekani na kusisitiza kuwa Washington katika miongo kadhaa sasa imekuwa ikitoa maagizo kwa nchi nyinginezo duniani kuhusu eti namna zinavyopasa kuamiliana na maandamano katika nchi hizo. 

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imeeleza kuwa madai ya kutetea haki za binadamu yanayotolewa na viongozi wa Marekani kufuatia hali ya ndani ya nchi hiyo ni ya kufedhehesha  kwa sababu polisi ya nchi hiyo inawakandamiza na kutumai mabavu dhidi ya wananchi wanaoandamana kwa kuwatumia askari wa nguvu ya ziada na kwa kustafidi na nyenzo mahsusi na gesi ya kutoa machozi. 

Maria Zakharova Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia pia ametahadharisha kuhusu kuendelea kukiukwa haki za binadamu nchini Marekani. Miji mbalimbali ya Marekani imekuwa ikishuhudia maandamano ya wananchi wanaopinga vitendo vya ubaguzi wa rangi vya polisi wa nchi hiyo. Maandamano hayo ambayo pia yameenea katika nchi nyingi za Ulaya yalianza mara baada ya polisi mmoja mzungu wa Marekani kumuua kikatili Mmarekani mwenye asili ya Afrika kwa jina George Floyd katika mji wa Minneapolis jimboni Minnesota tarehe 25 mwezi Mei mwaka huu. 

George Floyd alivyouliwa kikatili na polisi mbaguzi wa rangi nchini Marekani  

Tags