Maelfu wamuomboleza Floyd huku mashinikizo ya kufanyika mageuzi nchini Marekani yakiongezeka
Maelfu ya waombolezaji nchini Marekani wametoa heshima zao za mwisho kwa George Floyd aliyefia aliyeuawa na polisi, hatua ambayo imeibua maandamano makubwa kote nchini humo dhidi ya vitendo vya utumiaji mabavu na ubaguzi wa rangi dhidi ya raia wa nchi hiyo wenye asili ya Afrika.
Waombolezaji wamefika katika kanisa moja huko Houston jimboni Texas kumuenzi na kutoa heshima zao za mwisho kwa George Floyd, Mmarekani mwenye asili ya Afrika aliyeuliwa kikatili wiki iliyopita na polisi mbaguzi mzungu huko Minneapolis. Maombolezo haya ni awamu ya mwisho ya shughuli za kutoa heshima kwa mwendazake ambazo zimekuwa zikifanyika kabla ya kuzikwa leo katika mji alikozaliwa.
George Floyd aliyekuwa na umri miaka 46 aliaga dunia baada ya kukabwa shingoni kwa goti na polisi mzungu kwa jina la Derek Chauvin kwa muda wa dakika tisa huko Minneapolis jimboni Minnesota Mei 25 mwaka huu.

Kifo cha kikatili cha raia huyo Mmarekani mweusi mwenye asili ya Afrika kimeibua maandamano makubwa nchini Marekani na katika nchi nyingine huku watu wakiendelea kupinga vitendo vya mabavu vya polisi na ubaguzi wa rangi nchini Marekani.