Matumaini baada ya watafiti kugundua dawa ya kutibu corona
Matumaini yameenea kote duniani baada ya watafiti katika Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza kutangaza kile walichokitaja kuwa ni ‘hatua kubwa' katika kuwatibu wagonjwa wa COVID-19 au corona.
Watafiti hao wamebaini kuwa dawa aina ya steroidi dexamethasone ina uwezo wa kuepusha hatari ya kifo miongoni mwa wagonjwa mahututi.
Utafiti uliofanywa kwa zaidi ya wagonjwa 2,000, umeonyesha kuwa dawa hiyo ilipunguza hatari ya mgonjwa kufa kutoka asilimia 40 hadi asilimia 28, haswa wagonjwa ambao hawangeweza kupumua bila usaidizi wa mashine.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa taarifa na kutangaza kufurahishwa na matokeo ya awali ya najaribio ya dawa hiyo ya kutibu corona Uingereza
Kwa wagonjwa wanaotumia mashine za kupumua, dawa hiyo ilionesha kwamba imepunguza idadi ya vifo kwa theluthi moja, na kwa wagonjwa wanaohitaji hewa ya oksijeni, idadi ya vifo ilipungua kwa humusi au moja ya tano kulingana na matokeo ya awali yaliyotolewa na WHO.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema hii ndio dawa ya kwanza kupunguza idadi ya vifo kwa wagonjwa wa virusi vya corona wanaohitaji oksijeni au walio kwenye mashine za kupumua.
Dexamethasone ni dawa ambayo imekuwa ikitumiwa kwa muda kupunguza uvimbe katika hali tofauti kama vile ugonjwa wa saratani, yabisi kavu na kadhalika.
Hadi sasa hakuna chanjo ambayo imepatikana kukabili virusi vya corona.
Ugonjwa wa COVID-19 uliibuka kwa mara ya kwanza Disemba mwaka 2019 mjini Wuhan nchini China na sasa umeenea kote duniani.
Idadi jumla ya walioambukizwa COVID-19 duniani hadi kufikia Alhamisi hii ilikuwa ni takribani milioni 7.94 na waliopoteza maisha ni zaidi ya 535,000.
Marekani inaongoza duniani kwa maambukizi na vifo vya corona ambapo hadi kufikia leo watu zaidi ya milioni 2. 8 walikuwa wameambukizwa COVID-19 na wengine wasiopungua 119,000 wamepoteza maisha.