Katibu Mkuu wa UN ataka serikali za dunia ziwasaidie wajane
https://parstoday.ir/sw/news/world-i61783-katibu_mkuu_wa_un_ataka_serikali_za_dunia_ziwasaidie_wajane
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa mwito kwa serikali za nchi mbali mbali duniani kutowatelekeza wajane na badala yake zitoe kipaumbele kwa maslahi ya tabaka hilo la wanawake katika mipango yao ya kufufua chumi za nchi zao zilizoathiriwa na janga la corona.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 23, 2020 23:29 UTC
  • Katibu Mkuu wa UN ataka serikali za dunia ziwasaidie wajane

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa mwito kwa serikali za nchi mbali mbali duniani kutowatelekeza wajane na badala yake zitoe kipaumbele kwa maslahi ya tabaka hilo la wanawake katika mipango yao ya kufufua chumi za nchi zao zilizoathiriwa na janga la corona.

Antonio Guterres alitoa mwito huo jana Jumanne katika ujumbe wake alioutoa kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Wajane iliyoadhimishwa hiyo jana katika pembe mbali mbali za dunia.

Sehemu moja ya ujumbe huo wa Guterres inasema: Siku ya Kimataifa ya Wajane mwaka huu inaadhimishwa katika hali ambayo, idadi ya vifo vya wagonjwa wa COVID-19 inaendelea kuongezeka katika sehemu mbali mbali duniani, hususan (vifo vya) wanaume. Hii ni fursa nzuri ya kuelekeza darubini katika upande wa mgogoro (wa corona) ambao aghalabu umesahaulisha maisha pamoja na muskabali wa wajane walioachwa nyuma baada ya vifo vya waume zao.

Katibu Mkuu wa UN amekumbusha kuwa, "vifo vya wanaume katika wakati wowote ule vinaweza kuwaacha wanawake pasina haki ya kurithi mali. Katika nyakati za majanga, hasara hizi huwa maradufu kwa wajane ambao pia huandamwa na unyanyapaa na kubaguliwa."

Jamii nyingi huwatelekeza wajane na kuwaachia mzigo wa kuwalea mayatima

Guterres ametamatisha ujumbe wake huo kwa kusema, "katika maadhimisho haya ya Siku ya Kimataifa ya Wajane, tushirikiane katika kuzipa nguvu jamii zetu, thamani za familia, na tuzijenge upya jamii zetu zitakazowasaidia wajane katika kila nyanja.

Siku ya Kimataifa ya Wajane huadhimishwa Juni 23 kila mwaka, kwa lengo la kuakisi, kujadili na kutafuta njia za kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayowakabili mamilioni ya wawawake waliofiwa na waume zao.