Binti wa Luther King awataka Wamarekani kuendeleza maandamano ya kupinga ubaguzi
(last modified Wed, 24 Jun 2020 13:15:30 GMT )
Jun 24, 2020 13:15 UTC
  • Bernice King
    Bernice King

Binti wa aliyekuwa kiongozi wa harakati ya kupigania haki za kiraia za Wamarekani wenye asili ya Afrika, Martin Luther King, amewataka raia wa nchi hiyo waendeleze maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi nchini Marekani hadi uadilifu utakapotendeka.

Bernice King ambaye alikuwa akihutubia watu walioshiriki katika shughuli ya maziko ya Rayshard Brooks, Mmarekani mweusi aliyeuawa kwa kupigwa risasi na polisi mzungu huko Atlanta, amewataka Wamarekani kuendeleza maandamano ya kupinga ubaguzi na ukatili wa polisi.

Bernice King ameongeza kuwa, Wamarekani hawataacha maandamano na malalamiko yao hadi pale kilio chao kitakaposikilizwa na matakwa yao ya kufanyika marekebisho katika ngazi zote za jeshi la polisi yatakapotekelezwa.

Rayshard Brooks

Rayshard Brooks alipigwa risasi na polisi mzungu katika mji wa Atlanta hapo tarehe 12 mwezi huu wa Juni. Mauaji ya raia huyo wa Marekani mwenye asili ya Afrika yamechochea zaidi maandamano na ghasia za kupinga ubaguzi na ukatili wa polisi nchini Marekani zilizoanza baada ya polisi mwingine mzungu kumuua George Floyd katika mji wa Minneapolisi tarehe 25 Mei.