Vita vya biashara kati ya China na Marekani
(last modified Sun, 16 Aug 2020 09:54:37 GMT )
Aug 16, 2020 09:54 UTC
  • Vita vya biashara kati ya China na Marekani

Beijing na Washington leo zinatarajiwa kubadilishana mawazo na kutathmini sehemu ya kwanza ya mapatano yao ya kibiashara.

Kwa mujibu wa mapatano yaliyofikiwa tarehe 15 Januari mwaka huu, pande mbili hizi zilipanga kufanya mazungumzo baina ya viongozi wa ngazi za juu wa Marekani na China kila baada ya miezi sita. Kwa msingi huo iwapo mazungumzo hayo yatafanyika leo, hilo litakuwa tukio muhimu ambalo litazipa pande zote mbili fursa ya kuchunguza na kutathmini maendeleo yaliyopatikana katika mazungumzo ya biashara ya pande mbili.

Mazungumzo ya leo yanachukuliwa kuwa na umuhimu mkubwa kwa kutilia maanani kwamba mwezi mmoja tu baada ya kufanyika mazungumzo ya Januari 15, Marekani ilianzisha hujuma kali ya kibiashara dhidi ya China na hata kudai kwamba virusi vya corana ambavyo hivi sasa vimeikumba dunia nzima vilienea ulimwenguni kutokana na uzembe wa viongozi wa Beijing. Ni kutokana na suala hilo ndipo wataalamu wengi wa wakaamini kwamba kuongezeka mivutano ya hivi karibuni kati ya nchi mbili hizo kunaweza kuharibu matunda yote yaliyopatikana katika uwanja wa biashara. Kuhusu suala hilo, jarida la Sputnik limesema kwamba hatua za kulipizana kisasi pande mbili kama vile kufungiana balozi ndogo katika miji ya nchi mbili zinaweza kuwa na taathira mbaya sana katika uhusiano wa nchi hizo na hivyo kuharibu maendeleo yaliyopatikana katika uwanja wa biashara.

Vita vya biashara baina ya China na Marekani

Shaka kuhusu kufaniwa mazungumzo ya hivi sasa imeongezeka katika hali ambayo Marekani imekuwa na matumaini makubwa ya kuweza kupunguza pengo la mabadilishano ya biashara baina yake na China, ambalo ni la mamia ya mabilioni ya dola. Katika hatua ya kwanza ya mazungumzo ya kibiashara kati ya nchi hizo, China ilikuwa imekubali kununua bidhaa za dola bilioni 200 kutoka Marekani katika kipindi cha miaka miwili ili kupunguza pengo hilo.

Ni wazi kuwa wasiwasi wa Marekani katika vita vyake vya kibiashara na China hauishii katika suala hilo bali, jarida la Fortune hivi karibuni liliorodhesha mashiriki 500 makubwa ya kibiashara duniani ambapo kwa mara ya kwanza China imeishinda Marekani kwa kuwa na mashirika yenye mapato makubwa zaidi ulimwenguni. Jarida hilo limeandika: 'Tokea wakati wa kuanza kuorodheshwa mashirika 500 bora zaidi duniani kwa msingi wa mapatano yao mnamo mwaka 1995 hadi leo, kulikuwa hakujawahi kushuhudiwa ustawi wa haraka wa aina hiyo. Hii ni katika hali ambayo kabla ya hapo, mashirika mengi yaliyopata fursa ya kuorodheshwa kwenye orodha hiyo ya mshirika 500 bora kwa msingi wa mapatano yao ya kila mwaka, yalikuwa ni ya Marekani, lakini hivi sasa China imeweza kuchukua nafasi hiyo kwa kuwa na mshirika mengi zaidi bora duniani.'

Mbali na hayo gazeti la mtandaoni la Spiegel pia limeandika kuwa siasa za chokochoko za Marekani zimefanya hali ya mambo kuwa ngumu kwa marafiki zake wa Mashariki ya Mbali. Linasema: 'Vita vya biashara na mgogoro wa kidiplomasia unaotokana na kufungwa kwa balozi ndogo, hali ya Hong Kong na shirika la Huawei ni baadhi ya mambo ambayo yamezididha mvutano wa Marekani na China, mvutano ambao unazidi kuongezeka kila siku. Hali hiyo imeiweka Japan katika hali ngumu sana.'

IMF

Jambo lisilo na shaka ni kuwa, tokea mwanzoni mwa mwaka huu, mvutano wa Marekani na China umekuwa ukiongezeka, lakini pamoja na hayo uchumi wa China umekuwa ukiendelea kustawi kwa kasi kubwa na hivyo kuufanya kukaribia kuwa injini ya uchumi wa dunia. Katika utabiri wake wa karibuni kuhusu ustawi wa uchumi mwaka huu wa 2020, Mfuko wa Fedha wa Kimataifa IMF umetabiri kuwa uzalishaji ghafi wa ndani duniani utapungua kwa asilimia 5 na kwamba wa chumi zilizoendela kama vile za Marekani, eneo la Euro, Japan, Canada na Uingereza utapungua kwa asilimia 8 na kuwa nchi pekee ambayo uchumi wake utakuwa kwa tarakimu chanya ni wa china ambapo utaongezeka kwa asilimia moja.

Kwa ujumla ni kwamba kwa kuzingatia ukuaji mkubwa na wa kasi wa uchumi wake, tena katika mazingira ambayo chumi kubwa za dunia ukiwemo wa Marekani, eneo la Euro na Japan zingali ziko kwenye mdodoro, ni wazi kuwa madai ya China kuongoza uchumi wa dunia ni ya kweli, hivyo nafasi za madola makubwa katika ngazi za kimataifa zinaendelea kubadilika.