UN: Muungano wa Saudia ungali unaishambulia Yemen kwa mabomu yaliyopigwa marufuku
Umoja wa Mataifa umeeleza katika ripoti kuwa, muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia unatumia mabomu yaliyopigwa marufuku ya vishada katika mashambulio yake dhidi ya mji wa al Hudaydah, magharibi mwa Yemen.
Katika ripoti yake hiyo, Umoja wa Mataifa umekosoa vikali utumiaji huo wa mabomu ya vishada unaofanywa na muungano vamizi wa kijeshi wa Saudia nchini Yemen.
Utumizi wa mabomu ya vishada umepigwa marufuku kwa mujibu wa makubaliano kuhusu silaha za vishada yaliyopitishwa mwaka 2008.
Hadi sasa, ndege za kivita za muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia zimeshatumia mara kadhaa mabomu ya vishada kwa ajili ya kushambulia miji ya Yemen.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetahadhrisha kuwa kuwepo mabomu ya vishada nchini Yemen ambayo bado hayajaripuka kumeyageuza baadhi ya maeneo ya nchi hiyo "uwanja wa mabomu ya kutegwa ardhini".
Mnamo mwezi Machi 2015, Saudi Arabia, ikiungwa mkono na Marekani, Imarati na nchi zingine kadhaa iliivamia kijeshi Yemen na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa kila upande. Moto wa vita uliowashwa na Saudia na waitifaki wake nchini Yemen hadi sasa umesha sababisha makumi ya maelfu ya watu kuuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.
Uvamizi wa kijeshi wa Saudia umeisababishia pia nchi masikini ya Yemen uhaba mkubwa wa chakula na dawa.../