Vizuizi vinavyokwamisha kuanza mazungumzo ya amani ya Afghanistan
(last modified Sat, 05 Sep 2020 02:31:02 GMT )
Sep 05, 2020 02:31 UTC
  • Vizuizi vinavyokwamisha kuanza mazungumzo ya amani ya Afghanistan

Safari ya ujumbe unaoiwakilisha serikali ya Afghanistan katika mazungumzo ya amani na kundi la Taliban, ambao ulikuwa uondoke Kabul kuelekea mjini Doha, Qatar imeakhirishwa.

Ijapokuwa hakujatolewa maelezo yoyote kuhusu sababu ya kuakhirishwa safari ya ujumbe huo, lakini kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Afghanistan, Naibu Mkuu wa Baraza Kuu la Maslahi ya Taifa la Afghanistan amesema, safari ya ujumbe wa serikali katika mazungumzo ya amani imesogezwa mbele hadi siku chache zijazo.

Kwa sasa, suali linaloulizwa ni, mambo gani hasa ndiyo yanayokwamisha kuanza mazungumzo ya amani ya Afghanistan? Na je, mazungumzo hayo yataweza kuanza mnamo siku chache zijazo huko nchini Qatar? Kwa mujibu wa baadhi ya vyombo vya habari, mazungumzo baina ya Waafghani yataanza wiki ijayo nchini Qatar; na ilivyopangwa, Abdullah Abdullah, Rais wa Baraza Kuu la Maslahi ya Taifa la Afghanistan ataelekea huko kwa mwaliko aliopewa na serikali ya Doha; lakini jambo lililo wazi ni kwamba, kwa hivi sasa mazungumzo ya amani ya Afghanistan yanakabiliwa na matatizo matatu makuu:

Tatizo la kwanza linalotatiza mazungumzo ya amani ya Afghanistan ni tofauti za mitazamo zilizomo ndani ya serikali yenyewe ya Afghanistan.

Rais Ashraf Ghani (kulia) na Abdullah Abdullah Mkuu wa Baraza Kuu la Maslahi ya Taifa la Afghanistan

Hata kama serikali ya Afghanistan na makundi ya kisiasa yanakubaliana kwa kauli moja kuhusu mazungumzo hayo ya kutafuta suluhu na kurejesha amani nchini humo, lakini Rais Muhammad Ashraf Ghani na Abdullah Abdullah wanatofautiana katika uteuzi wa wajumbe wa timu itakayowakilisha serikali katika mazungumzo ya Qatar. Kwa maneno mengine, Abdullah Abdullah anaitakidi kuwa, kwa mujibu wa makubaliano ya kisiasa aliyofikia na Ashraf Ghani, uteuzi wa wajumbe wa Baraza Kuu la Maslahi ya Taifa la Afghanistan katika mazungumzo hayo, uko kwenye mamlaka yake yeye Rais wa baraza hilo.

Kwa mtazamo wa wataalamu wengi wa mambo, hata kama uteuzi wa wajumbe ni suala la ndani ya Afghanistan, lakini katika kadhia ya mazungumzo ya suluhu na kurejesha amani nchini humo, ambayo inahitaji uteuzi wa ujumbe wenye watu madhubuti na wa kitaifa kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Taliban, inapasa upatikane mshikamano wa ndani na umoja wa kitaifa; kwa hiyo hatua ya Ashraf Ghani ya kuteua watu anaowataka yeye itazidisha mpasuko na mgawanyiko kati ya shakhsia wa kisiasa, kikabila na kimadhehebu wa Afghanistan, hali ambayo Taliban inaichukulia kama turufu yake ya ushindi.

Lakini mbali na hilo, mtazamo wa kutaka kuhodhi kila kitu ilionao Taliban kuhusiana na mazungumzo ya amani ni tatizo la pili linalotatiza mazungumzo hayo ya kutafuta suluhu na amani ya Afghanistan. Kwa mtazamo wa weledi wengi wa mambo, Taliban inadai kwamba, iko tayari kwa mazungumzo ya amani ya mjini Doha, lakini ingali inatilia mkazo misingi na idiolojia yake ya kimadhehebu na kisiasa. Weledi hao wa mambo wanasema, ung’ang’anizi wa Taliban juu ya jambo hilo, maana yake ni kutaka ijikumbie fursa nyingi kadiri iwezekanavyo katika mazungumzo.

Maafisa waandamizi wa kundi la Taliban

Lakini licha ya uchu huo wa fursa ilionao Taliban, mkuu wa ujumbe wa wawakilishi wa serikali ya Afghanistan amesisitiza kuwa, katiba ya nchi ni mstari mwekundu wa mazungumzo na Baraza Kuu la Ushauri la Loya Jorga limeshaainisha dira na mipaka ya mamlaka ya upitishaji maamuzi unayopasa kuwa nayo ujumbe wa serikali katika mazungumzo ya amani.

Tatizo la tatu katika mazungumzo ya amani ya Afghanistan linahusu mtazamo wa kimaslahi alionao rais wa Marekani Donald Trump.

Lisilo na shaka ni kuwa Marekani ina mtazamo wa kiundumakuwili kuhusu mazungumzo ya amani ya Afghanistan. Kwa upande mmoja, vyombo vya habari vya Marekani vimeanzisha kampeni mpya ya kuuchafua mchakato wa amani ya Afghanstan, lakini kwa upande mwingine Trump ameonyesha kuwa na dhamira ya kuyatumia mazungumzo ya amani ya nchi hiyo kama moja ya turufu zake katika uchaguzi wa rais wa Marekani.

Arif Sahar, mtafiti wa masuala ya usalama wa kimataifa na mapambano dhidi ya ugaidi ana haya ya kunena kuhusiana na nukta hiyo: “Marekani haijaonyesha kuwa mkweli na yenye mwamana unaotakikana katika kutekeleza hati ya makubaliano ya Qatar; na badala yake imeanzisha mchezo wa ulaghai wa kisiasa ndani ya Afghanistan na kimataifa ili kuitumia karata ya amani ya Afghanistan katika uchaguzi ulioko mbele yake.”

Kwa ujumla inapasa tuseme kuwa, hata kama serikali ya Afghanistan na kundi la Taliban zimefikia makubaliano ya kuhitimisha vita na mapigano, lakini mazungumzo baina ya pande hizo mbili hayajaweza kuanza hadi sasa kwa sababu kadhaa. Na inavyoonekana, sababu kuu ya kuakhirishwa mazungumzo ya amani ya Afghanistan inatokana na muamala wa kindumakuwili wa serikali ya Trump.

Trump alipokutana na Ashraf Ghani

Wakati Trump na serikali yake wanataka kuyatumia kimaslahi mazungumzo ya amani ya Afghanistan, wananchi wenyewe na weledi wa kisiasa ndani ya Afghanistan wanaamini kuwa, mazungumzo ya amani yanaweza kuwa na mafanikio kwa msingi wa makundi na vyama vyote vya siasa kukubali kufungamana na misingi mikuu ya sheria za nchi hiyo ikiwemo katiba, ili kuweza kuwa na fungu katika mgao wa madaraka ya nchi. Na sababu ni kwamba historia ya Afghanistan ni mithili ya kioo kinachoakisi taswira za kushindwa na kuporomoka watu waliotaka kushika hatamu za utawala wa nchi hiyo bila uungaji mkono wa wananchi, bali kwa kutegemea msukumo wa madola ya kigeni; Afghanistan ambayo, ina umaarufu katika fasihi ya siasa wa kujulikana kama lindi la kuzikia na kufukia watawala majabari…/