Waliouawa katika zilzala ya Izmir, Uturuki wapindukia 50
https://parstoday.ir/sw/news/world-i64376-waliouawa_katika_zilzala_ya_izmir_uturuki_wapindukia_50
Idadi ya watu waliopoteza maisha kwenye maafa ya tetemeko la ardhi lililotokea mjini Izmir nchini Uturuki imeripotiwa kufika 51, huku timu za uokoaji zikiendelea kutafuta manusura na maiti zilizokwama chini ya vifusi vya nyumba na majengo yaliyobomolewa na zilzala hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 02, 2020 00:59 UTC
  • Waliouawa katika zilzala ya Izmir, Uturuki wapindukia 50

Idadi ya watu waliopoteza maisha kwenye maafa ya tetemeko la ardhi lililotokea mjini Izmir nchini Uturuki imeripotiwa kufika 51, huku timu za uokoaji zikiendelea kutafuta manusura na maiti zilizokwama chini ya vifusi vya nyumba na majengo yaliyobomolewa na zilzala hiyo.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya Makamu wa Rais wa Uturuki, Fuat Oktay na Kituo Kikuu cha Kukabiliana na Majanga nchini humo. Taarifa hiyo inasema kuwa, mbali na watu 51 kupoteza maisha katika tetemeko hilo la Ijumaa, wengine 896 wamejeruhiwa.

Maeneo yaliyoko magharbi mwa Uturuki Ijumaa iliyopita yalikumbwa na mitetemeko kadhaa ya ardhi iliyofikia ukubwa wa 6.6 kwa kipimo cha Rishta.

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki hiyo jana aliwasili katika eneo la tukio na kukagua mabaki ya jengo moja lililoporomoka kutokana na tetemeko hilo la ardhi liliutikisa mkoa wa Izmir.

Timu za uokoaji zikiendelea kutafuta manusura na maiti zilizokwama chini ya vifusi vya nyumba na majengo Izmir

Kituo cha Kupambana na Maafa na Dharura cha Uturuki  (AFAD), kimesema tetemeko hilo la ardhi la ukubwa 6.6 kwa kipimo cha Rishta lilihisika umbali wa kilomita 17 wilayani Seferihisar ndani ya mkoa wa Izmir, ambao upo katika pwani ya Bahari ya Aegean. 

Kadhalika tetemeko hilo la ardhi lililoripotiwa kufikia kina cha kilomita 16.54 ardhini limesababisha maafa katika nchi jirani ya Ugiriki.