Marekani yajiondoa rasmi katika Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Paris
Marekani hii leo imejiondoa rasmi katika Makubaliano ya Mabadiliko ya Tabianchi yaliyofikiwa mjini Paris, Ufaransa mwaka 2015.
Wadadisi wa mambo wanasema hatua ya leo inayoashiria kukamilika mchakato wa mwaka mzima wa kujiondoa Marekani katika mkataba huo wa kimataifa, itaipelekea Washington itengwe zaidi na kijamii ya kimataifa.
Mwaka 2017, Rais Donald Trump alitangaza kuiondoa Marekani katika muafaka huo wa kimataifa, akisisitiza kuwa makubaliano hayo hayana faida yoyote kwa nchi yake.
Wanasayansi wameonya kuwa, hatua ya Marekani ya kujiondoa katika mkataba huo itaisababishia sayari ya dunia ongezeko kubwa la joto kali, hasa kwa kuzingatia kuwa, Marekani ndio chanzo kikuu cha kuongezeka joto hilo duniani.
Kwa mtazamo wa Trump, kimsingi suala la ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya tabianchi ni mambo yasiyo na ukweli wowote na kwamba eti mambo hayo yamebuniwa tu na Wachina.
Hii ni katika hali ambayo, mwishoni mwa mwaka jana, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema kuwa, joto kali linaloendelea kushuhudiwa duniani huenda likashindakana kulidhibiti ikiwa hatua za dharura hazitochukuliwa kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.