Nov 07, 2020 07:19 UTC
  • Mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Cuba wakutana Havana

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambaye yuko nchini Cuba kwa ziara rasmi, amekutana na kufanya mazungumzo na mwenzake wa Cuba Bruno Rodriguez.

Katika mkutano huo, wawili hao wamezungumza kuhusu uimarishwaji wa uhusiano wa nchi mbili katika nyuga za kisiasa, kiuchumi na kimataifa.

Aidha wamejadili uungaji mkono wa nchi mbili kwa kadhia ya Palestina na pia ushirkiano katika sekta za kawi, nanoteknolojia, bioteknolojia, na hali kadhalika ushirikiano katika masuala yanayohusu Amerika ya Latini na Asia Magharibi.

Mapema, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alitembelea  kituo cha utafiti wa utengenezaji dawa mjini Havana na vituo vingine vya sayansi katika mji huo mkuu wa Cuba.

Akiwa katika vituo hivyo, Zarif amefahamishwa kuhusu hatua ambazo Cuba imechukua katika kuunda chanjo kadhaa ikiwemo chanjo ya COVID-19.

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela (kulia) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohamad Javad Zarif

Kabla ya kuwasili Cuba Zarif alitembelea Venezuela ambapo alifanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo akiwemo Rais Nicolas Maduro. 

Siku ya Jumatano Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliwasili katika eneo la Amerika ya Latini kwa ajili ya ziara rasmi ya kuzitembelea nchi za Venezuela, Cuba na kisha Bolivia.

Akiwa Bolivia, Zarif anatazamiwa kuhudhuria sherehe ya kuapishwa rais mpya wa nchi hiyo Luis Arce.

Tags