Erdogan: Uturuki inataka kuwa na uhusiano mzuri zaidi na Israel
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema nchi yake ingependa iwe na uhusiano mzuri zaidi na Israel na kwamba mazungumzo yanaendelea baina ya pande mbili katika ngazi ya intelijensia.
Erdogan aliyasema hayo jana mbele ya waandishi wa habari baada ya Sala ya Ijumaa mjini Istanbul. Pamoja na hayo alikosoa pia sera za utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusiana na Wapalestina akisema "hazikubaliki."
Rais wa Uturuki amesema, nchi yake ina matatizo na wale aliowaita "watu walio katika ngazi ya juu" Israel na akaongeza kwamba, kama isingekuwa matatizo yao na watu hao uhusiano wa Uturuki na utawala wa Kizayuni ungelikuwa "tofauti sana".
Katika kutetea hatua ya serikali yake ya kufanya mazungumzo ya kiintelijensia na utawala haramu wa Kizayuni, Erdogan amedai: "Sera ya Palestina ni mstari wetu mwekundu. Haiwezekani sisi tukubali sera za Israel kuhusu Palestina."
Pamoja na hayo, mshauri wa rais huyo wa Uturuki Mesut Hakkı Caşın alitangaza siku ya Jumanne iliyopita kwamba, endapo Israel itaonyesha nia njema, karibuni hivi nchi hiyo itafungua tena ubalozi huko Tel Aviv katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Ikumbukwe kuwa Uturuki lilikuwa taifa la kwanza lenye Waislamu wengi kuutambua utawala bandia wa Kizayuni wa Israel mnamo mwaka 1949.
Mikwaruzano baina ya pande hizo mbili ilishtadi mwaka 2018, ambapo katika kulalamikia mashambuizi ya kinyama ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza na hatua ya Marekani ya kuuhamishia Baitul Muqaddas ubalozi wake uliokuwa Tel Aviv, Uturuki ilimwita nyumbani balozi wake aliyekuweko Tel Aviv na pia kumtimua balozi wa utawala wa Kizayuni wa mjini Ankara.../