UN yataka wahusika wa mauaji ya raia 100 Niger wakamatwe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kusikitishwa kwake na mashambulio mawili ya megenge ya wabeba silaha huko nchini Niger, yaliyopelekea watu wasiopungua 100 kuuawa.
Katika taarifa, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa UN amelaani vikali hujuma hizo za juzi Jumamosi, sambamba na kunyoosha mkono wa pole kwa familia za wahanga wa mashambulio hayo, serikali na taifa la Niger kwa ujumla.
Amesema ana imani kuwa serikali ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika itawasaka na kuwafikisha mbele ya sheria waliohusika na mashambulio hayo; na kuongeza kuwa UN itaendelea kusimama na kuliunga mkono taifa hilo katika mapambano dhidi ya ugaidi, magenge yenye misimamo ya kufurutu ada, na uhalifu wa kuratibiwa.
Wakati huohuo, Allesandra Morelli, mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) nchini Niger amelaani vikali mauaji hao ya kutisha ya raia wasio na hatia, akitaja ukatili huo kama shambulio dhidi ya jamii zenye amani.
Amesema shirika hilo linafanya jitihada za kuwapa msaada wa dharura ukiwemo ushauri nasaha mamia ya wakazi wa vijiji vilivyoshambuliwa katika hujuma hizo za Januari 2, waliolazimika kuyambikia makazi yao. Amesema aghalabu ya wanavijiji hao wameathirika kisaikolojia kutoka na mashambulio hayo.
Siku ya Jumamosi, magenge hayo yanayosadikika kuwa ya kigaidi yalishambulia vijiji viwili na kuua watu wasiopungua 100 na kujeruhi makumi ya wengine katika mpaka wa Niger na Mali.
Duru za habari zinaarifu kuwa, magaidi hao walishambulia vijiji vya Tchombangou na Zaroumdareye, katika mpaka wa magharibi wa Niger na Mali.