Jan 13, 2021 10:30 UTC
  • Hatua mpya ya serikali ya Trump dhidi ya Cuba

Ikiwa ni katika kudumisha siasa zake za uhasama dhidi ya serikali za mrengo wa kushoto katika eneo la Amerika ya Latini, serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani kwa mara nyingine imelirejesha jina la Cuba katika orodha ya nchi zinazodaiwa kuunga mkono ugaidi.

Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekai ametoa sababu ya kuchukuliwa hatua hiyo kuwa ni inatokana na Cuba kuwapa hifadhi raia wa Marekani waliokimbilia nchini humo na pia hatua ya Havana ya kumuunga mkono Rais Nicolas Maduro wa Venezuela.

Cuba imerudishwa tena kwenye orodha hiyo katika siku za mwisho mwisho za utawala wa Donald Trump katika hali ambayo serikali ya rais huyo mwenye utata, yenyewe imetekeleza mauaji makubwa ya kigaidi duniani katika miaka ya karibuni. Mauaji ya kinyama yaliyotekelezwa na serikali ya Washington katika nchi za Afghanistan na Syria ni ushahidi tosha katika uwanja huo. Hata ndani ya Marekani kwenyewe, matukio ya hivi karibuni baada ya kufanyika uchaguzi wa rais na hasa kuvamiwa Congress ya nchi hiyo na wahuni wanauongwa mkono na Trump, ni thibitisho tosha kwamba nara zinazotolewa na watawala wa Marekani za eti kuunga mkono demokrasia na kupambana na ugaidi ni uongu mtupu na kuwa nchi hiyo ni muungaji mkono mkubwa wa ugaidi ndani na nje ya mipaka yake. Ni wazi kuwa madai ya kutetea demokrasia ni chombo tu kinachotumiwa na watawala hao kwa ajili ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine.

Mike Pompeo

Marekani imechukua hatua hiyo dhidi ya Cuba katika hali ambayo ni miaka mingi sasa ambapo imekuwa ikiishinikiza serikali ya Havana kwa mbinu tofauti na sasa baada ya kushindwa kuiondoa madarakani serikali hali ya Venezuela, inatumia kisingizio cha Cuba kuunga mkono serikali ya Caracas kwa ajili ya kutoa mashinikizo zaidi dhidi ya nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo Cuba imekuwa ikikosoa siasa za Marekani kwa miaka mingi na kuzichukulia kuwa ni mfano wa wazi wa uungaji mkono ugaidi wa kimataifa. Shambulio la karibuni dhidi ya ubalozi wa Cuba nchini Marekani na viongozi wa nchi hiyo kutowajibika wala kuchukua hatua zozote za kufuatilia suala hilo ni mfano wa wazi katika uwanja huo.

Carlos Fernandez de Cossio, mmoja wa viongozi wa ngazi za juu katika serikali ya Cuba ameashiria historia ndefu ya ugaidi wa Marekani dhidi ya nchi yake na pia ushirikiano wa Marekani na watu na vile vile makundi yanayotekeleza ugaidi dhidi ya Cuba kutokea ardhi ya Marekani na kusema: Kwa hakika Cuba ni mmoja wa wahanga wa ugaidi.

Ni wazi kwamba upinzani mkali wa Cuba na Venezuela dhidi ya siasa za mabavu za utawala wa Trump zimeupelekea utawala huo kutumia mbinu tofauti kutoa mashinikizo ya kiuchumi dhidi ya nchi hizo ili kuzilazimisha ima zisalimu amri mbele ya Marekani au zikabiliwe na hatari ya kuondolewa madarakani. Katika kulaani siasa hizo za Marekani dhidi ya nchi huru za Amerika ya Latini, Rais Miguel Diaz-Canel wa Cuba amesema kuwa Marekani inafuatilia siasa za kupora maliasili za baharini za nchi hizo. Siasa za uadui za Marekani zinatekelezwa dhidi ya mataifa huru duniani katika hali ambayo jamii ya kimataifa imezitaka nchi zote zishirikiane na kuondoa vikwazo vya kiuchumi na hasa vinavyohusiana na bidhaa muhimu zikiwemo dawa, katika kipindi hiki cha kuenea virusi vya corona duniani, ili kuziwezesha serikali kukabiliana na janga hilo linalotishia maisha ya wanadamu.

Rais Miguel Diaz-Canel wa Cuba

Kwa kurejesha tena jina la Cuba katika orodha ya nchi zinazodaiwa kuunga mkono ugaidi, katika siku za mwisho za utawala wake, Trump anafanya juhudi za kufunika kushindwa kwake katika kuzikandamiza serikali za mrengo wa kushoto katika eneo la Amerika ya Latini.

Hii ni katika hali ambayo jamii ya kimataifa na hata wanasiasa wengi ndani ya Marekani kwenyewe, wanataka siasa za uhasama wa nchi hiyo dhidi ya Cuba na Venezuela zitazamwe upya katika serikali ijayo ya nchi hiyo.

Tags