Russia: Magaidi wanapanga kufanya 'shambulio bandia la kemikali' Syria
Serikali ya Russia imetahadharisha kuwa, kuna mpango wa kufanywa shambulizi bandia la silaha za kemikali katika mkoa wa Idlib nchini Syria.
Admeri Alexander Karpov, Naibu Kamanda wa Kituo cha Kuvipatanisha Vyama vya Upinzani Syria cha Wizara ya Ulinzi ya Russia amesema serikali ya Moscow ina ushahidi kuhusu njama hizo zinazolenga kuipaka matope serikali ya Damascus.
Amesema wanamgambo wa genge la kigaidi la Hayat Tahrir al-Sham wanapanga kufanya hujuma hiyo ya kuigiza ya kemikali za sumu katika kijiji cha Kabana mkoani Idlib na kisha wailaumu serikali ya Rais Bashar al-Assad wa nchi hiyo.
Mara kadhaa huko nyuma, nchi za Magharibi bila kutoa ushahidi wowote, zimekuwa zikiilaumu serikali ya Damascus kwa mashambulio ya kuigiza ya kemikali zilizopigwa marufuku eti dhidi ya raia wa Syria.
Itakumbukwa kuwa, mwaka 2018, Marekani, Ufaransa, Uingereza na baadhi ya nchi washirika wake ziliituhumu serikali ya Syria kwamba imetekeleza shambulizi la silaha za kemikali mjini Douma karibu na mji wa Damascus, ambapo kufuatia tuhuma hizo ziliishambulia nchi hiyo ya Kiarabu bila ya idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Serikali ya Syria sambamba na kukadhibisha madai hayo iliitisha wachunguzi wa kujitegemea wa kimataifa kwa ajili ya kwenda kufanya uchunguzi wao eneo hilo, ambapo ripoti zilionyesha kutojiri shambulizi hilo.