IAEA yataka washiriki wa JCPOA wakumbatie fursa waliyopewa na Iran
(last modified Wed, 17 Mar 2021 06:33:08 GMT )
Mar 17, 2021 06:33 UTC
  • IAEA yataka washiriki wa JCPOA wakumbatie fursa waliyopewa na Iran

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA amesema makubaliano ya nyuklia ya Iran ni 'magumu lakini yanatekelezeka' huku akizitaka pande husika za JCPOA kukumbatia muhula wa miezi mitatu ziliopewa na Jamhuri ya Kiislamu kwa ajili ya kuyanusuru mapatano hayo.

Akizungumza kwa njia ya video jana Jumanne mbele ya kamati tatu za Bunge la Ulaya, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Rafael Grossi alisema si muhali kwa Marekani kurejea katika makubaliano ya nyuklia ya Iran, lakini pande mbili zinahitaji kuandaliwa mazingira ya mazungumzo.

Grossi amenukuliwa na shirika la habari la Associated Press akisema kuwa, "Wao (Marekani) wanataka kurejea (katika makubaliano hayo), lakini bila shaka kuna baadhi ya masuala yanayopaswa kutatuliwa. Kwa hiyo si muhali, ni vigumu lakini si jambo lisilowezekana."

Mwezi uliopita, Grossi aliitembelea Tehran na kufanya mazungumzao na maafisa wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika mazungumzo hayo ilitangazwa kuwa Iran itasimamisha utekelezaji wa Protokali ya Ziada; na Grossi kwa upande wake akatangaza kuwa anaitambua haki ya serikali ya Iran ya kutekeleza sheria iliyopitishwa na bunge la nchi hii kwa ajili ya kukabiliana na vikwazo vya kidhalimu.

Grossi na Salehi katika mkutano wa huko nyuma hapa Tehran

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (AEOI), Ali Akbar Salehi alisema kuhusu mapatano yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya Iran na wakala huo kwamba, kwa muda wa miezi mitatu, IAEA haitakuwa na haki ya kuangalia kamera na mifumo ya kurekodia taarifa; na kama vikwazo havitaondolewa katika miezi mitatu ijayo, taarifa hizo zitafutwa na kamera za wakala huo wa nishati ya atomiki zitaondolewa.

Itakumbukwa kuwa, kwa muda wa mwaka mzima tangu Marekani ilipojitoa kinyume cha sheria katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Iran iliendelea kutekeleza kikamilifu majukumu yake katika makubaliano hayo na ikazipa fursa nchi za Ulaya zilizoahidi kuchukua hatua ya kufidia athari za kujitoa huko kwa Marekani kutekeleza ahadi zao.

Tags