Maandamano ya kupinga kufungwa nchi yafanyika katika nchi za Ulaya
Maafisa wa polisi katika nchi kadhaa za Ulaya wamekosolewa kwa kutumia nguvu kupita kiasi kuzima maandamano ya wananchi wanaopinga maagizo mapya ya serikali za nchi hizo yaliyotangazwa kwa ajili kuzuia msambao wa wimbi la tatu la virusi vya Corona.
Maandamano hayo yalianzia katika jiji la Kassel katikati mwa Ujerumani na London, mji mkuu wa Uingereza kabla ya kuenea katika miji mingine ya nchi mbili hizo na nyinginezo kadhaa za Ulaya.
Msemaji wa Polisi katika jiji la Kassel nchini Ujerumani amesema watu zaidi ya 20,000 walishiriki maandamano hayo ya jana ambayo yanahesabiwa kubwa makubwa zaidi mwaka huu nchini humo. Hata hivyo maafisa usalama walitumia mabomu ya kutoa machozi na virungu kuyazima.
Waandamanaji hao sawa na wenzao katika miji mingine ya nchi hiyo wanalalamikia hatua ya serikali kufunga nchi na kuweka vizuizi vya kutoka nje na mijumuiko kama njia moja wapo ya kudhibiti wimbi la tatu la msambao wa ugonjwa wa Covid-19.
Makumi ya watu wametiwa mbaroni katika maandamano hayo ya nchini Ujerumani na katika mji mkuu wa Uingereza, London.
Kadhalika maandamano kama haya yameshuhudiwa katika nchi nyingine za Ulaya kama vile Austria, Ubelgiji, Croatia, Finland, Poland, Romania, Sweden na Uswisi.
Nchini Finland, mbali na kulalamikia sheria mpya za kudhibiti msambao wa Corona, lakini mamia ya waandamanaji wamesikika wakipinga kampeni ya chanjo dhidi ya Covid-19 na uvaaji barakoa wa lazima.