Balozi wa Marekani nchini Russia aitwa kurejea nyumbani
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetangaza kwamba imemtaka balozi wake aliyeko mjini Moscow Russia arejee nyumbani kwa mashauriano zaidi na viongozi wa Washington.
Wizara hiyo imesema kwamba Balozi John Sullivan ametakiwa arudi mjini Washington wiki hii kwa ajili ya kufanya mashauriano na viongozi wa serikali mpya ya Rais Joe Biden ambao inadaiwa hajapata nafasi muafaka ya kuonana nao tokea alipochaguliwa katika nafasi hiyo ya kuhudumia serikali ya Marekani mjini Moscow, na vile vile kuonana na familia yake.
Pamoja na hayo lakini wajuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa kuna sababu nyingine nyingi na muhimu zaidi ambazo zimempelekea Balozi John Sullivan aitwe nyumbani mjini Washington. Serikali ya Marekani Alkhamisi iliyopita iliwawekea vikwazo vipya raia na mashirika 32 ya Russia.
Serikali ya Washington imesema imetekeleza vikwazo hivyo vipya dhidi ya raia na mashirika ya Russia kwa hoja kuwa nchi hiyo iliingilia uchaguzi mkuu uliopita wa Marekani kupitia hujuma za kimtandao. Imeamua pia kuwafukuza nchini humo wanadiplomasia 10 wa Russia kutokana na tuhuma hizo hizo.
Katika kutoa jibu kwa hatua hiyo ya Marekani, viongozi wa Russia nao wamewafukuza nchini humo wanadiplomasia 10 wa Marekani na kuwaweka viongozi wanane wa Marekani katika orodha ya vikwazo ya Russia.
Uhusiano wa Marekani na Russia umeharibika katika miaka ya karibuni kutokana na mambo tofauti yakiwemo ya tuhuma za Marekani dhidi ya Russia kuwa inaingilia mambo ya ndani ya Ukraine.