Malalamiko yaendelea Marekani kupinga ubaguzi na ukandamizaji wa polisi
Maandamano yanaendelea katika jimbo la Carolina Kaskazini nchini Marekani kulaani ubaguzi wa rangi na ukandamizaji wa jeshi la polisi la nchi hiyo baada ya kuuliwa na polisi, Mmarekani mwengine mwenye asili ya Afrika kwenye jimbo hilo.
Televisheni ya CNN ya Marekani imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, maandamano yanaendelea katika mji wa Elizabeth wa Carolina Kaskazini kwa siku kadhaa sasa tangu siku ya Jumatano, kulalamikia mauaji ya kikatili yaliyofanywa na polisi dhidi ya Andrew Brown, Mmarekani mwenye asili ya Afrika.
Andrew Brown (40) alikuwa baba wa watoto 10 na alipigwa risasi na polisi akiwa ndani ya gari lake, siku ya Jumatano iliyopita, yaani siku moja tu tangu alipopatikana na hatia afisa mwingine wa polisi mbaguzi wa rangi. Afisa huyo ni Derec Chauvin, ambaye alimuua kikatili na mchana kweupe, Mmarekani mwengine mwenye asili ya Afrika, George Floyd.
Baada ya kupita wiki tatu za vikao vya kusikiliza ushahidi wa upande wa mashitaka na mshtakiwa, jopo la majaji waliokuwa wakisikiliza kesi ya George Floyd, Jumanne iliyopita lilitangaza kuwa Chauvin amepatikana na hatia katika mashitaka matatu ya mauaji yaliyokuwa yakimuandama.
Hukumu dhidi ya afisa huyo mzungu wa Marekani inatazamiwa kusomwa katika kipindi cha wiki nane zijazo, na huenda atahukumiwa kifungo cha miongo kadhaa jela.
Jumatatu iliyopita siku moja kabla ya majaji kutoa tangazo la kumpata na hatia Chauvin mwenye umri wa miaka 45, maandamano makubwa yalikuwa yanaendelea nje ya mahakama na katika maeneo mengine ya mji wa Minneapolis kutaka uadilifu utendeke.