Taliban wateka bwawa muhimu huku mapigano makali yakiwa yanaendelea Afghanistan
Kundi la Taliban limeteka bwawa la pili kwa ukubwa na umuhimu nchini Afghanistan katika mapigano makali na vikosi vya jeshi la serikali kwenye mkoa wa Kandahar huku jeshi vamizi la Marekani likiwa limeanza kuwaondoa askari wake tangu ilipoivamia kijeshi nchi hiyo miaka 20 iliyopita.
Maafisa wa mkoa huo wameyathibitishia mashirika ya habari kuwa bwawa la Dahla, linalotumiwa na wakulima kwa ajili ya umwagiliaji na pia kwa matumizi ya maji ya kunywa katika mji wa Arghandab makao makuu ya jimbo hilo, limetekwa na kundi hilo.
Msemaji wa Taliban Qari Yousu Ahmadi, naye pia amethibitisha taarifa hiyo akisema: "Tunalishikilia bwawa la Dahla katika eneo la Arghandab."
Bwawa hilo limetekwa na kundi la Taliban baada ya mapigano kuzuka katika mkoa jirani wa Helmand mapema wiki hii, siku chache baada ya jeshi vamizi la Marekani kuanza kuwaondoa rasmi askari wake nchini Afghanistan.
Mkuu wa Idara ya Maji ya mkoa wa Kandahar Tooryalay Mahboobi amevieleza vyombo vya habari kuwa, hivi karibuni, kundi la Taliban lilitoa onyo kwa wafanyakazi wa bwawa la Dahla kutoenda kazini.
Katika mkoa jirani wa Helmand, maelfu ya watu wameyakimbia makazi yao kutokana na mashambulio makubwa ya Taliban dhidi ya vikosi vya serikali.
Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa mwaka jana mjini Doha, Qatar kati ya Marekani na Taliban, hadi kufikia Mei mosi mwaka huu, askari wote wa Marekani ilipasa wawe wameshaondoka katika ardhi ya Afghanistan, hata hivyo Washington ilisogeza tarehe hiyo hadi Septemba 11, hatua ambayo imelikasirisha kundi hilo.
Kuondoka kwa majeshi vamizi ya kigeni nchini Afghanistan kunafanyika huku jitihada za kufikiwa makubaliano ya amani kati ya kundi la Taliban na serikali ya Afghanistan zikiwa zimegonga mwamba hadi sasa.../