Ajali ya treni yasababisha vifo vya makumi ya watu nchini Pakistan
Takriban watu 40 wameaga dunia na zaidi ya 120 wamejeruhiwa baada ya kugongana kwa treni mbili karibu na mji wa kusini mwa Pakistani wa Daharki.
Ajali hiyo iliyokea jana Jumatatu karibu na mji wa Daharki, umbali wa kilomita 440 kaskazini mwa jiji kubwa la Karachi.
Afisa mwandamizi wa polisi ya Daharki, Umar Tufail alisema watu 40 wameaga dunia katika ajali hiyo.
Idadi ya waliokufa huenda ikaongezeka kutokana na idadi kubwa ya majeruhi wa ajali hiyo na jitihada zilikuwa zikiendelea za kukwamua watu walionasa kwenye mabehewa ya treni hizo.
Ajali hiyo ilitokea wakati mabehewa nane ya treni ya kaskazini ya Millat Express yalipotoka nje ya reli karibu na eneo la Daharki. Maafisa wa eneo hilo wanasema treni ya abiria ya Sir Syed Express ya kusini iligonga mabehewa yaliyopinduka ya treni nyingine.
Waziri Mkuu wa Pakistani Imran Khan amesema "ameshtushwa" na ajali hiyo, na amemwamuru Waziri wa Reli, Azam Swati kuelekea eneo la ajali hiyo.
Mfumo wa reli uliochaa wa Pakistan umesababisha ajali nyingi katika miaka ya hivi karibuni, na serikali ya nchi hiyo inalaumiwa kwa kutowekeza vya kutosha kwa ajili ya kuboresha huduma za usafiri wa reli.
Mwaka wa 2019, watu wasiopungua 73 walifarikii dnia baada ya mtungi wa gesi kulipuka ndani ya treni iliyokuwa imejaa abiria karibu na mji wa Liaquatpur.