Mamia waaga dunia kutokana na joto kali nchini Canada
(last modified Wed, 30 Jun 2021 11:20:11 GMT )
Jun 30, 2021 11:20 UTC
  • Mamia waaga dunia kutokana na joto kali nchini Canada

Mamia ya watu wamefariki dunia nchini Canada baada ya joto lisilo la kawaida kushuhudiwa katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

Polisi ya eneo la British Columbia imepokea taarifa za vifo vipatavyo 70 tangu Jumatatu, vilivyotokana na joto ambalo limevunja rekodi ya kiwango cha joto la kawaida.

Baadhi ya maafisa wa serikali katika mkoa wa British Columbia unaojumuisha mji wa Vancouver wamesema watu wapatao 233 wameaga dunia katika eneo hilo kati ya Jumatatu na Ijumaa kutokana na joto kali.

Jana Jumanne, kiwango cha joto nchini Canada kiliongezeka zaidi kwa siku ya tatu mfululizo, huku nyuzijoto 49.5 ikinakiliwa katika maeneo ya Lytton na British Columbia. Kabla ya wiki hii , kiwango cha joto cha Canada hakikuwahi kuvuka nyuzijoto 45.

Umoja wa Mataifa: Ongezeko la viwango vya joto duniani ni ishara ya wazi ya mabadiliko ya tabianchi ya muda mrefu

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini humo imetahadharisha kuwa, kiwango hicho cha joto kinaweza kuwa hatari kwa jamii ya watu ambao hawajiwezi hasa wazee na wale wenye matatizo ya kiafya. Kwa mujibu wa polisi , joto hilo linaaminika kuwa limesababisha vifo vya watu 69 katika mji wa Vancouver wilaya ya Burnaby. 

Hivi karibuni, Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani WMO lilitoa tahadhari kwamba joto la kupita viwango vya wastani litarajiwe kwenye sehemu nyingi duniani katika miezi michache ijayo.