Taliban: Tutaunda utawala wa Kiislamu utakaoshirikisha Waafghani wengine pia
Msemaji wa kundi la Taliban ametaka iundwe serikali ya Kiislamu nchini Afghanista inayoendana na mazingira itakayojumuisha na Waafghani wengine pia.
Suhail Shaheen ameyasema hayo leo katika mji mkuu wa Qatar, Doha na kusisitiza kuwa serikali mpya itakayoundwa nchini Afghanistan haitahusisha wanachama wa kundi hilo peke yao.
Shahen ameongeza kuwa Taliban inataka shakhsia mbalimbali maarufu wa Afghanistan washiriki katika serikali mpya itakayoundwa na kundi hilo.
Halikadhalika msemaji huyo wa Taliban amesema, kundi hilo litawahakikishia usalama wanajeshi na askari wa vikosi vya usalama watakaokabidhi silaha zao na kujiunga na kundi hilo.
Kabla ya tangazo hilo, viongozi wa Taliban waliliambia gazeti la Times la Uingereza kuwa kundi hilo haliafiki wazo la kuundwa serikali ya mpito nchini Afghanistan.
Wapiganaji wa kundi la Taliban, jana Jumapili Agosti 15 waliingia mji mkuu wa Afghanistan, Kabul sambamba na kuanguka kwa serikali kufuatia hatua ya Rais Muhammad Ashraf Ghani kuitoroka nchi.../