Kadhaa wauawa katika maandamano ya 'bendera' nchini Afghanistan
Kwa akali watu watatu wameuawa huku makumi ya wengine wakijeruhiwa katika maandamano ya kulalamikia kitendo cha wapiganaji wa Taliban kuondoa bendera ya taifa hilo na kuweka bendera ya kundi hilo katika maeneo muhimu ya mji wa Jalalabad, mashariki mwa Afghanistan.
Kwa mujibu wa televisheni ya al-Jazeera ya Qatar, watu hao wameuawa kwa kupigwa risasi kwa kupinga kuwekwa bendera yenye nembo ya Taliban katika moja ya medani muhimu katika mji huo wa mashariki mwa nchi, mkoani Nangarhar.
Maelfu ya watu wamejitokeza mabarabarani kushiriki maandamano hayo ya kuonyesha uungaji mkono wao kwa bendera ya taifa, huku wakilalamikia vikali kubadilishwa bendera hiyo kwa ile ya Taliban.
Habari zaidi zinasema kuwa, maandamano kama hayo yameshuhudiwa katika mikoa na miji mingine ya nchi hiyo, mbali na jiji la Jalalabad lililoko yapata kilomita 150 mashariki mwa mji mkuu, Kabul.
Wakati huohuo, mashirika ya Umoja wa Mataifa yametoa wito kwa utawala wa Taliban nchini Afghanistan kutekeleza ahadi zake za kuwalinda wananchi.