Uingereza yaidhinisha dawa ya kuzuia na kutibu Corona
https://parstoday.ir/sw/news/world-i73742-uingereza_yaidhinisha_dawa_ya_kuzuia_na_kutibu_corona
Mamlaka ya Kusimamia Dawa na Matibabu Uingereza (MHRA) imeidhinisha kile ilichokitaja kuwa dawa ya aina yake ya kukinga na kutibu ugonjwa wa COVID-19.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 20, 2021 21:58 UTC
  • Uingereza yaidhinisha dawa ya kuzuia na kutibu Corona

Mamlaka ya Kusimamia Dawa na Matibabu Uingereza (MHRA) imeidhinisha kile ilichokitaja kuwa dawa ya aina yake ya kukinga na kutibu ugonjwa wa COVID-19.

Serikali ya Uingereza kupitia taasisi hiyo imeidhinisha matumizi ya mchanganyiko wa dawa za kuimarisha kinga ya mwili unaoitwa Ronapreve, ikisisitiza kuwa dawa hiyo ina uwezo wa kuzuia na hata kuponya ugonjwa wa Corona. 

Sajid Javid, Waziri wa Afya wa Uingereza amesema serikali ya London ikishirikiana na wadau wengine katika sekta ya afya inafanya kila linalowezekana kuona kuwa dawa hiyo inaingia masokoni haraka iwezekanavyo ili kupiga jeki vita dhidi ya janga hilo la kimataifa.

Haya yanajiri mwaka mmoja baada ya watafiti katika Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza kutangaza kile walichokitaja kuwa ni ‘hatua kubwa' katika kuwatibu wagonjwa wa COVID-19, kwa kudai kuwa dawa aina ya Steroidi Dexamethasone ina uwezo wa kuepusha hatari ya kifo miongoni mwa wagonjwa mahututi.

Hii ni katika hali ambayo, licha ya Uingereza na nchi nyingine kadhaa duniani kutangaza kupata dawa za kutibu Corona, lakini ugonjwa huo hatari unaendelea kuihangaisha jamii ya mwanadamu kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa.

UK yasumbuliwa na Corona licha ya 87% ya watu milioni 66 wa nchi hiyo kupigwa chanjo

Februari mwaka jana, China ilitangaza kuwa dawa ya kutibu wagonjwa walioathiriwa na virusi hatari vya Corona imepatikana nchini humo kutokana na juhudi za timu ya watafiti katika maabara ya Zijiang. Miezi minne baadaye, Wizara ya Afya ya Russia ilitangaza kwamba imepasisha dawa nyingine iliyopewa jina la Levilimab kwa ajili ya kutibu wagonjwa mahututi wa Corona.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, serikali ya Uganda iliidhinisha matumizi ya dawa ya mitishamba ya 'Covidex' kwa ajili ya kutibu magonjwa ya virusi ukiwemo ugonjwa wa COVID-19.