Johnson: Tutaendelea kufanya mazungumzo na Taliban
Waziri Mkuu wa Uingereza amesema hakuna uhusiano wowote kati ya Daesh na Taliban na kueleza kuwa serikali ya Uingereza itaendelea kufanya mazungumzo na kundi la Taliban.
Boris Johnson amebainisha kuwa, Taliban kamwe si rafiki wa tawi la Khorasan la Daesh lililohusika na mashambulizi katika uwanja wa ndege wa Kabul. Waziri Mkuu wa Uingereza amekariri msimamo wake wa huko nyuma kwamba, kama kundi la Taliban linataka kufanya mazungumzo na nchi za Magharibi basi linapasa kuwaruhusu wananchi wa Afghanistan kuondoka nchini humo.
Maafisa wa tiba wa Afghanistan wametangaza kuwa watu 60 wameuawa na 140 katika milipuko miwili iliyotokea juzi Alhamisi mkabala wa uwanja wa ndege wa Kabul na mwingine katika hoteli ya Baron. Katika milipuko hiyo wanajeshi 13 wa Marekani wameuawa. Milipuko hiyo imetekelezwa sambamba na kukaribia tarehe 31 mwezi huu muhula uliotolewa na Rais Joe Biden wa Marekani wa kuwaondoa Afghanistan wanajeshi wa Marekani.
Vyombo vya habari vimetangaza kuwa, kundi la kigaidi la Daesh limekiri kuhusika na milipuko hiyo ya Kabul. Itakumbukwa kuwa, Uingereza ni kati ya nchi zilizomo kwenye Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (Nato) ambao imefeli huko Afghanistan. Uingereza imekosolewa sana ndani na nje ya nchi hiyo kwa kushindwa kwake huko Afghanistan baada ya kundi la Taliban kuidhibiti nchi hiyo.
Kuwepo kijeshi Marekani na waitifaki wake huko Afghanistan kwa muda wa miaka ishirini hakujakuwa na matunda yoyote ghairi ya kuzidisha ugaidi, vita, hali ya mchafukoge na kuuliwa makumi ya maelfu ya wananchi wa Kiafghani.