Kukaribia uundwaji wa serikali mpya ya Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i74104-kukaribia_uundwaji_wa_serikali_mpya_ya_afghanistan
Msemaji wa kundi la Taliban ametangaza kuwa, serikali mpya ya Afghanistan itaundwa katika kipindi cha wiki mbili zijazo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 31, 2021 02:23 UTC
  • Kukaribia uundwaji wa serikali mpya ya Afghanistan

Msemaji wa kundi la Taliban ametangaza kuwa, serikali mpya ya Afghanistan itaundwa katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

Zabihullah Mujahid, Msemaji wa Kundi la Taliban amesema, sambamba na kukaribia kumalizika oparesheni ya kuondoka wanajeshi wote wa Marekani nchini Afghanistan, kundi hilo sasa linajitayarisha kuunda serikali mpya.

Zabihullah Mujahid ameongeza kuwa, kuundwa serikali mpya kutapunguza matatizo ya nchi hiyo kama vile kupungua thamani ya sarafu ya kitaifa na kuvurugika uchumi.

Punde baada ya kundi la Taliban kuchukua udhibiti wa Kabul na kutoroka nchi Rais Ashraf Ghani, swali ambalo limekuwa likulizwa na wengi kitaifa, kieneo na kimataifa ni kuhusu muundo wa serikali mpya ya Afghanistan.

Pamoja na kuwa baada ya kuanguka serikali ya Rais Ashraf Gani mnamo Agosti 15 na aghalabu ya maeneo ya Afghanistan kudhibitiwa na Taliban, kundi hilo limekuwa likijaribu kuunda serikali jumuishi lakini hakujatolewa maelezo kuhusu serikali hiyo. Makundi  mbali mbali ya kisiasa, kikaumu na kimadhehebu nchini Afghanistan hayajaweza kufahamu Taliban wanataka kuunda vipi serikali jumuishi.

Zabihullah Mujahid, Msemaji wa Kundi la Taliban

Kuna taarifa rasmi na zisizo rasmi kuwa, Baraza la Kisiasa la Taliban linafanya mazungumzo na viongozi na wanaharakati wa kisiasa, kikaumu, na kimadhehebu kutoka kona zote za Afghanistan kuhusu suala hilo. Lakini pamoja na hayo, kuna wasi wasi kuwa yamkini Taliban hawatatekeleza ahadi wanazotoa za kuunda serikali jumuishi na badala yake kutashuhudiwa utawala wenye wafuasi wa Taliban pekee.

Nukta hii inapata nguvu hasa kwa kuzingatia kauli ya hivi karibuni ya msemaji wa Taliban kuwa katika kipindi cha wiki mbili zijazo serikali mpya itatangazwa Afghanistan. Wasi wasi uliopo unatokana na kuwa, makundi mengine bado hayajaweza kuwasilisha majina au mapendekezo kuhusu serikali hiyo inayotarajiwa kutangazwa.

Kwa kuzingatia matamshi ya Zabihullah Muhajidi, Msemaji wa Taliban kuwa kundi hilo sasa limebadilisha muelekeo na halina sifa kama zile za miaka 20 iliyopita na kwamba azma yake ni kuunda serikali yenye kuleta pamoja makundi mbali mbali ya Afghanistan, tarajio la watu na kaumu mbali mbali nchini humo ni kuwa Taliban imepata funzo na itawashirikisha wote katika mchakato wa kisiasa nchini humo.

Ashraf Ghani,Rais wa Afghanistan aliyetoroka nchi baada ya Taliban kuingia Kabul

Misimamo ya nchi mbali mbali duniani inaonyesha kuwa iwapo kundi la Taliban litaunda serikali ambayo itakuwa na wanachama wake tu basi dunia itapinga hatua hiyo na serikali kama hiyo itatengwa kimataifa.

Kwa msingi huo, viongozi wa Taliban wanapaswa kuwa na uwazi katika stratijia yao ya kuunda serikali mpya ya Afghanistan na wawabainishie watu wa nchi hiyo ni vipi wanataka kuunda serikali yenye kujumuisha makundi yote.