Ravanchi:Baraza la Usalama liilazimishe Israel ihitimishe kuikalia kwa mabavu Golan
-
Majid Takht-Ravanchi
Balozi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa Baraza la Usalama la umoja huo linalazimiika kutekeleze wajibu wake na kuulazimisha utawala wa Kizayuni wa Israel uache kuikalia kwa mabavu miinuko ya Golan na uvamizi dhidi ya Syria.
Akihutubia kikao cha Baraza la Usalama, Majid Takht-Ravanchi ameeleza kuwa, uvamizi na hatua za kuibua machafuko za utawala wa Israel ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa. Amesema vitendo hivyo vya utawala wa Kizayuni vinatishia usalama na amani ya kikanda na kimataifa.
Utawala haramu wa Israel mara kwa mara umekuwa unatekeleza mashambulizi ya makombora na kuvilenga vituo vya kijeshi huko Syria hususan vile vya harakati ya Hizbullah ya Lebanon. Hizbullah imekuwa na mchango mkubwa katika kulisaidia jeshi la Syria kupambana na magaidi wanaofadhiliwa na nchi ajinabi.
Israel imekuwa ikiyasaidia kwa hali na mali makundi ya kigaidi ambayo yanapigana dhidi ya serikali ya Rais Bashar al Assad tangu nchi ajinabi na makundi yao ya kigaidi yaanzishe uvamizi huko Syria miaka kumi iliyopita. Serikali ya Syria inasema kuwa utawala wa Kizayuni na waitifaki wake wa Magharibi na baadhi ya nchi za kanda ya Magharibi mwa Asia zinayasaidia kwa silaha na kifedha makundi ya kigaidi na kitakfiri ambayo yanatekeleza hujuma mbalimbali na kuvuruga amani nchini humo.
Wakati huo huo Israel inalikalia kwa mabavu eneo kubwa la miinuko ya Golan kusini magharibi mwa Syria tangu mwaka 1967; na hivyo kudumisha uwepo wake mkubwa kijeshi katika nchi hiyo ya Kiarabu.