Dec 02, 2021 07:27 UTC
  • WFP yatoa indhari: Hali ya kibinadamu Afghanistan ni mbaya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula WFP limesema, hali ya kibinadamu nchini Afghanistan ni mbaya na kutoa ombi maalum la kusaidia watu wa nchi hiyo bila kujali masuala ya kisiasa ya nchi hiyo.

Kupitia video maalumu ya zaidi ya dakika 5 pamoja na picha kadhaa ilizotoa kuionesha dunia hali mbaya ya kibinadamu inayoendelea nchini Afghanistan ikiwemo ya ukosefu wa chakula, WFP imesisitiza kuwa, wanaoteseka nchini humo ni raia wa kawaida; na watoto wenye utapiamlo mkali wanazidi kuongezeka wakati huu ambapo nchi hiyo inaingia kwenye msimu wa baridi kali.

Mwakilishi mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula nchini Afghanistan Mary-Ellen McGroarty amesema, kwa sasa jamii ya kimataifa inapaswa kuiangalia Afghanstan sio kwa jicho la kisiasa na nani anaongoza nchi hiyo bali kwa jicho la kibinadamu.

Bi McGroarty ameongezea kwamba: "Tunahitaji kutenganisha umuhimu wa msaada wa kibinadamu na majadiliano ya kisiasa. Watu wa Afghanistan, watu wasio na hatia wa Afghanistan, watoto wa Afghanistan ambao maisha yao yameharibiwa bila makosa yao wenyewe, hawawezi kuhukumiwa kwa njaa juu ya njaa kwa sababu tu ya bahati nasibu ya jiografia iliyowafanya wao kuzaliwa hapa".

Hayo yanaripotiwa huku Benki ya Dunia ikitangaza hivi karibuni kuwa inakamilisha taratibu za pendekezo ililotoa la kuipatia Afghanistan dola milioni 500 za fedha zake zilizozuiwa ili zitumike kama msaada kwa ajili ya nchi hiyo.../

Tags