Ershadi: Baraza la Usalama la UN liilazimishe Israel kuondoka Golan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i78284-ershadi_baraza_la_usalama_la_un_liilazimishe_israel_kuondoka_golan
Balozi na Naibu Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuwahami na kuwasaidia watu na serikali ya Syria kwa ajili ya kukomboa ardhi yao inayokaliwa kwa mabavu na amesisitiza kuwa Baraza la Usalama linapaswa kuulazimisha utawala haramu wa Israel kuondoka Golan na kukomesha uvamizi na uchokozi wake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 21, 2021 04:50 UTC
  • Zahra Ershadi
    Zahra Ershadi

Balozi na Naibu Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuwahami na kuwasaidia watu na serikali ya Syria kwa ajili ya kukomboa ardhi yao inayokaliwa kwa mabavu na amesisitiza kuwa Baraza la Usalama linapaswa kuulazimisha utawala haramu wa Israel kuondoka Golan na kukomesha uvamizi na uchokozi wake.

Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, Zahra Ershadi aliyasema hayo jana Jumatatu katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York kuhusu Syria. Aliongeza kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani vikali hujuma zote za utawala wa Israel dhidi ya Syria na inasisitiza haki ya asili ya Syria ya kujilinda."

Mwanadiplomasia huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Kuendelea kukaliwa kwa mabavu na majeshi ya kigeni sehemu za ardhi ya Syria ambako ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ni lazima kukomeshwe; na vikosi vyote vya kigeni vinavyozikalia kwa mabavu na vilivyoko nchini humo bila ya kualikwa, vinapaswa kuondoka haraka katika nchi hiyo bila masharti yoyote.

Balozi na Naibu Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema: "Ripoti ya hivi karibuni ya vyombo vya habari vya Marekani kuhusu mauaji yaliyofanywa na vikosi vya jeshi la Marekani dhidi ya makumi ya raia wa Syria, ikiwa ni pamoja na wakulima, watoto na wanakijiji, ambayo tuyanalaani vikali, inasisitiza udharura wa kuondolewa mara moja kwa vikosi hivyo vamizi kutoka Syria."

Jeshi vamizi la Marekani huko Syria

Ershadi amesema kuwa, mgogoro wa Syria lazima utatuliwe kwa amani na kwa mujibu wa kanuni na sheria za kimataifa, hasa zile zinazosisitiza kuheshimu kikamili mamlaka nchi mbalimbali.