Meli ya Kivita ya Uingereza yaelekea Libya kuzuia wahamiaji
Uingereza imetangaza kuwa itatuma meli ya kivita nchini Libya kuzuia wahamiaji wa kigeni ambao wanatumia pwani ya nchi hiyo kuvuka Bahari ya Mediterranean na kuiniga Ulaya kinyume cha sheria.
Akizungumza leo Ijumaa akiwa katika kikao cha viongozi wa nchi za kundi la G7, Waziri Mkuu wa Uingereza amedai kuwa meli hiyo ya kivita inatumwa Libya kwa ajili ya kukabiliana na wahamiaji haramu. Uingereza kama nchi zingine duniani inakabiliwa na tishsio la wahamiaji wanaoingia Ulaya kupitia nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Aidha amesema kuwepo kundi la kigaidi la ISIS au Daesh ni tishio kwa usalama wa Uingereza.
Maafisa wa Uingereza wanasema meli hiyo ya kivita itazizuia boti ambazo zinabeba wahamiaji haramu na silaha.
Mwezi uliopita Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Philip Hammond alisema nchi yake inaweza kutumia nguvu za kijeshi kusaidia serikali halali ya Libya ili kurejesha usalama nchini humo. Alisema Uingereza inatafakari pia kuanzisha mashambulizi ya anga dhidi ya magaidi wa ISIS ambao wanaudhubiti mji wa Sirte nchini Libya.
Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, mnamo Jumatano 25 Mei akizungumza katika kikao cha pamoja na waandishi habari na Waziri Mkuu wa Italia Matteo Renzi, alisema kuwa, NATO iko tayari kuingilia kijeshi nchini Libya.
Viongozi wa Libya wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kuwa hawataki vikosi vya kigeni nchini humo bali wanachohitaji ni msaada wa kimataifa wa silaha na mafunzo ya kijeshi ili kuweza kurejesha amani na utulivu nchini humo.