Iran: Marekani haina azma ya kufunga jela ya Guantanamo
(last modified Fri, 14 Jan 2022 02:53:35 GMT )
Jan 14, 2022 02:53 UTC
  • Iran: Marekani haina azma ya kufunga jela ya Guantanamo

Mkuu wa Masuala ya Kimataifa wa Idara ya Mahakama ya Iran ameukosoa vikali utawala wa Rais Joe Biden wa Marekani kwa kufeli kutekeleza ahadi yake ya kufunga jela ya kutisha ya Guantanamo Bay iliyoko nchini Cuba.

Kazem Gharib Abadi, ambaye pia ni Katibu wa Baraza Kuu la Haki za Binadamu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema hayo jana Alkhamisi katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, kwa mnasaba wa kuwadia mwaka wa ishirini tangu kuanzishwa jela hiyo ya kutisha ya Guantanamo.

Amesema si tu Marekani imekataa kutekeleza ahadi iliyotoa yenyewe ya kulifunga gereza hilo ambalo linawashikilia washukiwa kinyume cha sheria, lakini ina mpango wa kuipanua jela hiyo mwaka huu.

Afisa huyo mwandamizi wa kutetea haki za binadamu wa Iran amekumbusha kuwa, tangu jela ya Guantanamo ilipoanzishwa Januari 12, 2002, takriban watu 780 wameshikiliwa katika jela hiyo na hadi sasa tuhuma za kutenda uhalifu walizobambikiwa bado hazijathibitika. Gharib Abadi amesema wafungwa 39 wangali wanashikiliwa katika jela hiyo, iliyoko mashariki mwa Cuba katika eneo linalokaliwa kwa mabavu na Marekani.

Washukiwa wakiteswa katika jelala Guantanamo

Jumatatu iliyopita, wataalamu huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa pia waliitaka Marekani itekeleze ahadi yake ya kuifunga jela hiyo ya kutisha. Walisisitiza kuwa, miaka 20 ya uwepo wa jela hiyo inaashiria ukurasa wenye kuchukiza na kutisha wa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu wa Marekani.

Kabla ya hapo pia, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilitoa wito kwa Biden likimtaka atekeleze ahadi yake hiyo na kuifunga jela ya Guantanamo Bay mara moja.