Feb 21, 2022 01:13 UTC
  • Newsweek: Trump yumkini akafungwa jela miaka mitano

Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, huenda akafungwa jela miaka mitano kwa madai kwamba alichukua nyaraka za siri za Ikulu ya Rais wa Marekani kuhusiana na usalama wa taifa alipoondoka madarakani mwaka jana.

Katika ripoti yake, gazeti hilo limemnukuu Mwanasheria na Mkuu wa zamani wa Jeshi la Marekani, Glenn Kirschner akisema kuwa Trump anaweza kukabiliwa na mashtaka kadhaa katika siku za usoni kuhusiana na suala la nyaraka, na kusisitiza kwamba mtu mwingine yeyote anaweza kufunguliwa mashtaka kutokana na taarifa zilizopo.

Ripoti hiyo ilisema kuwa Idara ya Hifadhi ya Nyaraka na Kumbukumbu za Taifa ya Marekani ilisema katika barua yake ya Ijumaa iliyopita kwa Kamati ya Uangalizi ya Kongresi ya Marekani kwamba takriban masanduku 15 yaliyo na hati za siri za usalama wa kitaifa yalirudishwa na Trump mwezi uliopita, baada ya kutakiwa kufanya hivyo.

Trump anatuhumiwa kwamba amekuwa akihodhi taarifa hasasi, nyeti na hata za siri za serikali tangu wakati wa kipindi chake cha urais na hata baada ya kuondoka Ikulu ya White House.

Newsweek limewanukuu maafisa wa serikali wakisema kwamba hilo ni kosa la kuadhibiwa, na kwamba Idara ya Hifadhi ya Nyaraka na Kumbukumbu za Taifa ya Marekani, imeiarifu Wizara ya Sheria ambayo imeanza uchunguzi wa kadhia hiyo kwamba Trump alichukua nyaraka za siri za usalama wa taifa kutoka Ikulu ya White House na kuzihamishia Mar-Algo, huko Florida. Gazeti hilo limeripoti kuwa, kuweka nyaraka za siri ni uhalifu unaoadhibiwa kwa faini au kifungo kisichozidi miaka 5, au vyote kwa pamoja.

Donald Trump

Sheria ya serikali kuu ya Marekani inapiga marufuku kuzihamishia sehemu isiyoruhusika nyaraka za siri za serikali.

Hayo yanaripotiwa huku wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Marekani wakitaka wapatiwe taarifa za yaliyomo kwenye maboksi yaliyopatikana kwenye nyumba ya Trump ya Mar-a-Lago; hata hivyo idara hiyo ya nyaraka imesema sheria ya taarifa za kumbukumbu hairuhusu kutoa taarifa hizo.

Gazeti la Washington Post liliwahi kuripoti kuwa, afisa mmoja wa Mamlaka ya Hifadhi ya Nyaraka aliiomba Wizara ya Sheria kuchunguza ufichuzi wa maboksi 15 ya kumbukumbu za White House yaliyopatika kwenye nyumba ya rais huyo wa zamani wa Marekani huko Palm Beach Florida na kuongeza kuwa, alipokuwa White House, Trump alikuwa na mazoea ya kuchana aina zote mbili za nyaraka za kumbukumbu "nyeti na zisizo na umuhimu".

Tags