Feb 26, 2022 10:27 UTC
  • Mashariki ya Kati, ibra na somo la mgogoro wa Ukraine

Tarehe 25 mwezi huu wa Februari Russia ilipuuza propaganda na tahadhari za nchi za Magharibi na kuanzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Ukraine.

Mgogoro wa Ukraine unatoa somo na ibra mbili muhimu kwa nchi mbalimbali hususan za eneo Asia Magharibi.

Somo la kwanza la mgogoro huu ni suala la wazi lakini linaloendelea kupuuzwa na wengi. Wananadharia wa uhusiano wa kimataifa wanasema kuwa, nguvu zinategemea msingi na uwezo wa kijeshi. Kuwa na zana za kisasa za kijeshi na nguvu kazi bora na hodari ya kijeshi ni sehemu muhimu ya nguvu za nchi na taifa lolote lile. Wakati Muungano wa Kisovieti ulipoporomoka mwanzoni mwa miaka ya 1990, Ukraine ilikuwa nchi ya tatu duniani kwa kuwa na nguvu kubwa zaidi ya nyuklia ikiwa na vichwa 5,000 vya makombora ya nyuklia, lakini ilikabidhi silaha zake hizo kwa Russia kwa ajili ya kujaribiwa, hatua ambayo ilikuwa na maana ya kutoweka uwezo wa kujilinda wa Ukraine.

Balozi wa Ukraine mjini Tehran, Sergey Burdylyak anasema: "Nina uhakika kwamba kitendo cha kukabidhi silaha za nyuklia za Ukraine kwa Russia lilikuwa kosa la kisiasa na hatukupaswa kufanya kosa hilo." 

Nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zimeikimbia Ukraine wakati wa dhiki na shida

Mwanasiasa mashuhuri wa Ukraine, Yuriy Kostenko ameandika katika kitabu chake cha Ukraine's Nuclear Disarmament kwamba: "Sisi sote Waukraini tulidanganywa na tukafanya makubaliano hayo, kwa hivyo sote tumefanya makosa. Zoezi la kupokonywa silaha za nyuklia za Ukraine lilifanyika kwa mapatano na kupigiwa makofi na taifa la Ukraine na kuungwa mkono na vyombo vya habari. Hata hivyo sasa imebainika kuwa, tathmini hiyo ilikuwa ya makosa kikamilifu. Inaonekama kuwa, Ukraine imekuwa Iraq ya pili ambayo utawala wake uliondolewa madarakani kwa hujuma ya kimataifa." 

Somo la pili muhimu la mgogoro wa Ukraine hususan kwa eneo la Asia Magharibi ni matokeo ya kuamini na kuyategemea kupita kiasi madola ya Magharibi. 

Wananadharia wa mahusiano ya kimataifa wanaamini kuwa, asili na msingi wa usalama ni kujitegemea, na kila nchi inapaswa kulinda usalama wake yenyewe, kwa sababu hakuna nchi nyingine itakayojitolea kulinda usalama wake. Leo hii, nchi zote za Kiarabu wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi zimefungamanisha usalama wao na ahadi za madola ya Magharibi na zinayategemea kikamilifu kulinda usalama wao, kwa matumaini kwamba yatazilinda dhidi ya uvamizi wa kigeni. Mojawapo ya makosa makubwa ya kistratijia ya serikali ya Ukraine ni kupanga kete zake kwa kutegemea ahadi za nchi za Magharibi. Kilichobainika hadi sasa katika mzozo wa Ukraine na Russia ni kwamba, himaya ya nchi za Magharibi kwa Ukraine imebakia tu katika kuweka vikwazo vipya na vya aina mbalimbali dhidi ya Moscow, na nchi za Magharibi zinazoongozwa na Marekani hazitaingia vitani dhidi ya Russia kwa ajili ya Ukraine, kwa sababu hazioni maslahi yoyote ya kibinafsi katika suala hilo.

Raia wa Ukraine wakikimbilia usalama wao kwenye vituo vya usafiri wa treni ya chini ya ardhi

Jibu la nchi za Magharibi kwa hujuma na mashambulizi ya Russia dhidi ya Ukraine limebakia katika kutoa matamshi ya kukosoa na kueleza masikitiko tu. Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson amesema katika mazungumzo ya simu na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy kwamba ameshtushwa na yanayojiri nchini Ukraine na anatumai kuwa nchi hiyo inaweza kupambana. Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: “Ufaransa inalaani vikali uamuzi wa Russia wa kuanzisha vita dhidi ya Ukraine. Ufaransa inashikamana na Ukraine na itakuwa bega kwa bega na nchi hiyo.”

Rais wa Marekani Joe Biden, ameitishia Russia kwa vikwazo vikubwa, akisema dunia inaiombea Ukraine.

Mgogoro wa Ukraine umethibitisha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo inatilia mkazo suala la kuimarisha uwezo wake wa kijeshi na haiko tayari kufanya mazungumzo na madola ya Magharibi kuhusu uwezo wake wa kijeshi, iko kwenye njia sahihi.

Ukweli kuhusu mgogoro wa Ukraine ni kwamba, usalama si suala la kufanyiwa muamala wa aina yoyote. 

Tags