Maelfu ya wahajiri Waafghani wametelekezwa na Marekani makambini nchini Imarati
(last modified Wed, 02 Mar 2022 03:36:23 GMT )
Mar 02, 2022 03:36 UTC
  • Maelfu ya wahajiri Waafghani wametelekezwa na Marekani makambini nchini Imarati

Maelfu ya wahajiri Waafghani, ambao waliondolewa nchini mwao Afghanistan katika "Operesheni ya Uhamishaji" ya askari wa jeshi la Marekani wamebaki hawana mbele wala nyuma baada ya kupita karibu miezi saba tangu wahamishiwe katika Umoja wa Falme za Kiarabu, Imarati.

Wahajiri hao raia wa Afghanistan, waliohamishiwa kwenye kambi ya wakimbizi mjini Abu Dhabi nchini Imarati, wameilalamikia Marekani kwa kutojali hatima yao na kueleza: "walituahidi kuwa watatuhamisha kutupeleka Marekani ndani ya muda wa miezi miwili, lakini sasa imeshapita miezi sita hatujui la kufanya."

Wakimbizi hao Waafghani ambao idadi yao katika mji wa Abu Dhabi pekee wanakadiriwa kufika watu elfu kumi, walikuwa wakifanya kazi na wanajeshi wa Marekani na wa shirika la kijeshi la NATO; na waliwasaidia sana katika kutekeleza mipango ya Marekani nchini Afghanistan kwa muda wote wa miaka 20 iliyopita.

Waafghanistan wakiihama nchi yao kwa kutumia ndege ya jeshi la Marekani

Wakati huohuo, Naibu Kaimu Waziri Mkuu wa serikali ya muda ya Taliban Abdul Salam Hanafi ametuma salamu kwa wahajiri hao akisisitiza kuwa, wahajiri Waafghani ambao hawajui la kufanya huko waliko kwenye kambi za wakimbizi nje ya nchi, wanaweza kurudi nchini Afghanistan.

Msemaji wa Taliban Zabihullah Mujahid, naye pia amesema: "tunayo taarifa kwamba wakimbizi Waafghani, wakiwemo walioko Qatar na Uturuki wanaishi katika hali mbaya; na hiyo ndiyo sababu ya sisi kuwazuia watu hao wasiondoke nchini."

Wakati askari wa jeshi vamizi la Marekani walipokuwa wakiitoroka Afghanistan mwezi Agosti mwaka jana, Waafghani wapatao laki moja na elfu ishirini pia waliihama nchi hiyo.../