Wanaakademia wataka Vyuo Vikuu duniani visimame dhidi ya Israel
Makumi ya wasomi na wanaakademia wa Uingereza wametoa mwito kwa Vyuo Vikuu na taasisi zote za elimu ya juu kote duniani kusimama kidete mkabala wa kitendo cha utawala ghasibu wa Israel kukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina.
Katika barua yao ya wazi, wasomi hao kutoka miungano ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini Uingereza wameashiria kukaliwa kwa mabavu ardhi za Wapalestina kwa miongo mingi sasa, na kusisitiza kuwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu ni unakiuka sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa.
Wametoa mwito kwa Vyuo Vikuu na taasisi zote za elimu ya juu kote duniani kukata uhusiano na utawala wa Kizayuni, na badala yake ziwekeze huko Palestina.
Wanaakademia hao wa UK wamebainisha kuwa, hatua ya Vyuo Vikuu kuwekeza Israeal kwa ushirikiano na kampuni na mashirika ya utawala huo pandikizi ni kushirikiana moja kwa moja na Tel Aviv kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Mwezi uliopita, wanavyuo na wasomi 220 kutoka Vyuo Vikuu 14 ya Amerika ya Latini walilaani kitendo cha utawala haramu wa Israel cha kutekeleza mfumo wa ubaguzi wa rangi wa apartheid dhidi ya Wapalestina.
Walitoa mwito wa kutambuliwa Israel kama utawala wa mfumo wa apartheid, siku chache baada ya shirika la haki za binadamu la Amnesty International kuutaja utawala huo kama utawala wa kibaguzi.