Uturuki yalegeza kamba, yataka kufungwa faili la mauaji ya Khashoggi
Mwendesha Mashitaka wa Uturuki ameiomba mahakama ya nchi hiyo isimamishe kesi dhidi ya raia 26 wa Saudi Arabia wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa Washington Post, na mkosoaji mkubwa wa utawala wa Aal-Saud, Jamal Khashoggi, mwaka 2018.
Mahakama hiyo ya Uturuki jana Alkhamisi ilisema itatafuta miongozo na ushauri wa Wizara ya Sheria ya nchi hiyo, juu ya ombi hilo la kufungwa faili la mauaji ya Khashoggi. Kesi kuhusu ombi hilo imeratibiwa kusikilizwa Aprili 7.
Mwendesha Mashitaka wa Uturuki amesema kesi hiyo imekuwa ikiendeshwa kwa mwendo wa kobe kwa kuwa maagizo ya mahakama hayatekelezeki kwa msingi kuwa washukiwa ni raia wa kigeni. Kesi dhidi ya raia hao 26 wa Saudia imekuwa ikisikilizwa pasi na wao wenyewe kuwepo mahakamani.
Haya yanajiri wakati huu ambapo Uturuki imekuwa ikifanya jitihada za kuboresha uhusiano wake na Saudia, ambao ulidorora kufuatia mauaji hayo ya Khashoggi.
Jamal Khashoggi aliuliwa kikatili na kinyama mwaka 2018 ndani ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul, Uturuki na kikosi maalumu cha wauaji makatili kilichotumwa kutoka Saudia. Mwili wake uliokatwa vipande vipande na timu hiyo maalumu ya mauaji ya Saudia, haujapatikana hadi leo hii.
Nchi za Magharibi zinasema, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman ndiye aliyetoa amri ya kufanyika mauaji hayo. Mauaji hayo yaliushitua vibaya ulimwengu na kuharibu mno sura ya Saudi Arabia hususan mrithi wa kiti cha ufalme bin Salman na hasa nje ya nchi hiyo.