Uturuki yatangaza kusimamisha kesi ya Wasaudia 'waliomuua' Khashoggi
Mahakama moja nchini Uturuki imesimamisha kesi dhidi ya raia 26 wa Saudi Arabia wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa gazeti la Washington Post, na mkosoaji mkubwa wa utawala wa Aal-Saud, Jamal Khashoggi, mwaka 2018.
Mahakama hiyo ya mjini Istanbul imetangaza hayo jana Alkhamisi, licha ya mashirika ya kutetea haki za binadamu kuonya kuwa, kukabidhiwa faili la mauaji ya Khashoggi kwa utawala wa Riyadh kutapelekea kuyeyuka kwa kesi hiyo na kutowajibishwa kisheria wahusika wa mauaji hayo.
Haya yanajiri wiki moja baada ya Mwendesha Mashitaka wa Uturuki kuiomba mahakama ya nchi hiyo isimamishe kesi hiyo, ambayo ilikuwa inafanyika bila ya washukiwa hao wa Kisaudia kuwepo mahakamani.
Alisema kesi hiyo imekuwa ikiendeshwa kwa mwendo wa kobe kwa kuwa maagizo ya mahakama hayatekelezeki kutokana na ukweli kuwa washukiwa ni raia wa kigeni.
Baadhi ya duru za habari zinaarifu kuwa, Uturuki imeamua kufunga faili la mauaji ya Khashoggi kama sehemu ya jitihada zake za kuboresha uhusiano wake na Saudia, ambao ulidorora kufuatia mauaji hayo mwaka 2018.
Jamal Khashoggi aliuliwa kikatili mwaka 2018 ndani ya ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki na kikosi maalumu cha wauaji makatili kilichotumwa kutoka Saudia. Mwili wake uliokatwa vipande vipande na timu hiyo maalumu ya mauaji ya Saudia, haujapatikana hadi leo hii.
Nchi za Magharibi zinasema, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman ndiye aliyetoa amri ya kufanyika mauaji hayo.