Uturuki yaendeleza kampeni ya kutia nguvuni wahajiri
Serikali ya Uturuki imewatia nguvuni wahajiri wengine 232 katika mji wa Istanbul ukiwa ni mwendelezo wa kampeni ya kamatakamata dhidi ya wahamiaji.
Tangu ulipoanza mwaka 2021 hadi sasa, Uturuki imewazuia wahajiri wapatao laki sita kuingia nchini humo na ingali inaendelea kuchukua hatua kali za kiusalama katika mipaka yake kuzuia uingiaji wa wakimbizi na wahajiri.
Wakati wakimbizi wengi wanalazimika kuzihama nchi zao kwa sababu ya matatizo makubwa ya kiuchumi na kiusalama, takwimu rasmi zinaonyesha kuwa, mwaka uliopita Uturuki iliwazuia wakimbizi 451,096 kuingia nchini humo.
Tangu ulipoanza mwaka huu wa 2022 hadi tarehe 14 ya mwezi uliopita wa Aprili, askari usalama wa Uturuki wamewazuia wakimbizi 127, 256 kuingia nchini humo.
Shirika la habari la IRIB limeripoti kuwa, polisi ya Uturuki imewakamata wahajiri haramu 232 katika operesheni iliyofanywa katika maeneo mbalimbali ya mji wa Istanbul kwa madhumuni wa kuwanasa raia wa kigeni waliongia nchini humo kinyume cha sheria.
Watu 122 ambao imeamuliwa wahamishwe nchini Uturuki ni raia wa Afghanistan, 35 raia wa Syria, 14 raia wa Uzbekistan, tisa ni raia wa Pakistan na watu 52 ni raia wa nchi mchanganyiko.../