May 11, 2022 07:44 UTC
  • Jamhuri ya Czech yachukua nafasi ya Russia katika Baraza la Haki za Binadamu la UN

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limeipa Jamhuri ya Czech nafasi ya Russia baada ya kufuta uanachama wa Moscow kwenye baraza hilo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jana Jumanne lilipiga kura na kuipa Jamhuri ya Czech nafasi ya Russia katika Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo, kwa kura 157 za ndio na 23 za waliojiuziua kupiga kura.

Kipindi cha uanachama wa Jamhuri ya Czech kilianza jana Jumanne na kitamalizika tarehe 31 Disemba 2023 katika baraza hilo. Jamhuri ya Czech ilikuwa nchi pekee iliyopewa nafasi ya kugombea nafasi hiyo.

Tarehe 7 mwezi uliopita wa Aprili, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitisha kikao cha kusimamisha uanachama wa Russia katika Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo kutokana na vita vya Ukraine. Muswada huo ulipasishwa kwa kura 93 za ndio, 24 za hapana na 58 zilizojizuia kupiga kura.

Kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa

 

Katika zoezi hilo, nchi 24 zikiwemo Algeria, Belarus, Cuba, Korea Kaskazini, Iran, Kazakhstan, China, Russia, Syria, Uzbekistan, Tajikistan, Vietnam na kadhalika, zilipinga kusimamishwa uanachama wa Russia kwenye baraza hilo.

Nchi zilizopinga kusimamishwa uanachama wa Russia kwenye Baraza la Haki za Binadamu zinasema kuwa, Umoja wa Mataifa unaendesha siasa za kindumilakuwili katika kuamiliana na matukio mbalimbali duniani.

Nchi za Magahribi zinafanya jinai kubwa katika kila kona ya dunia, utawala wa Kizayuni wa Israel unafanya jinai za kutisha dhidi ya Wapalestina kwa makumi ya miaka sasa, wananchi wa Yemen wamefanyiwa ukatili mkubwa na vibaraka wa nchi za Magharibi kwa miaka mingi, lakini Umoja wa Mataifa haukuchukua hatua zozote dhidi ya madola hayo.

Tags