Polisi ya Japan yakiri uzembe ulisababisha kuuawa Shinzo Abe
Jeshi la Polisi nchini Japan limekiri kuwa udhaifu katika mipango ya usalama ulipelekea kuuawa waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo Shinzo Abe siku ya Ijumaa.
Mkuu wa polisi wa eneo la Nara Tomoaki Onizuka ameambia mkutano wa wanahabari, "hatuwezi kukataa kwamba kulikuwa na matatizo katika mpango wa usalama kutokana na jinsi mambo yalivyomalizika”. Tamko hilo limekuja baada ya walinzi wa Abe, ambao ni maafisa wa poilisi, kukoselewa vikali kutokana na uzemba wao katika kumlinda kiongozi huyo.
Abe alifariki dunia Ijumaa asubuhi baada ya kupigwa risasi mbili katika hujuma ya kigaidi wakati akiwa katika mkutano wa kampeni ya kisiasa katika eneo la Nara. "Ninahisi hisia kubwa ya kuwajibika," amesema, akiongeza kuwa polisi watachunguza tukio hilo na kutekeleza mabadiliko yoyote muhimu. Uchaguzi wa viti katika baraza la juu la bunge la Japan umefanyika kama ulivyopangwa leo Jumapili.

Matokeo ya uchunguzi wa maoni yanaonesha kuwa, kutokana na hisia za huzuni zinazotawala sasa nchini Japan, chama cha Shinzo Abe cha Liberal Democratic, kinatazamiwa kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi huo.
Uchunguzi huo wa maoni umeonyesha kwamba muungano unaotawala, chini ya uongozi wa Waziri Mkuu wa sasa wa Japan, Fumio Kishida, ambaye anatambuliwa kuwa mwanafunzi wa Abe, utashinda angalau viti 60 kati ya 125, ikilinganishwa na viti 55 unavyoshikilia kwa sasa.
Abe ambaye ana rekodi ya kipekee ya kuwa waziri mkuu aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi katika historia ya Japan, alijiuzulu nafasi hiyo mwaka 2020 kwa sababu za kiafya. Alikuwa Waziri Mkuu wa Japan kwa miaka 8 yaani tokea mwaka 2012 hadi 2020.