Onyo la China kwa Marekani iwapo Spika Pelosi atazuru Taiwan
(last modified Wed, 20 Jul 2022 02:19:16 GMT )
Jul 20, 2022 02:19 UTC
  • Nancy Pelosi
    Nancy Pelosi

China imeionya vikali Washington na kusisitiza kuwa itachukua 'hatua za nguvu' iwapo Spika wa Kongresi ya Marekani Nancy Pelosi atafanya safari ya kuitembelea Taiwan mwezi ujao wa Agosti.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Zhao Lijian alitoa indhari hiyo jana Jumanne na kueleza kuwa: China itatoa jibu la nguvu na mwafaka iwapo Pelosi atakizuru kisiwa cha Taiwan.

Amesema safari yoyote ya Pelosi katika eneo la Taiwan kama ilivyoripotiwa na gazeti la Financial Times itakuwa na matokeo mabaya katika uhusiano wa Beijing na Washington.

Lijian ameongezea kwa kusema: "Taiwan ni sehemu ya ardhi ya China na sisi hatuiruhusu nchi yoyote iingilie masuala yetu ya ndani." Ameitaka US ifute safari hiyo ya Pelosi kisiwani Taiwan, na iache kufanya mawasiliano rasmi na viongozi wa Taipei.

Pelosi hivi karibuni aliliambia gazeti la Financial Times la Marekani kuwa, atafanya safari ya kihistoria mwezi ujao wa Agosti katika eneo la Taiwan; ziara ambayo inatazamiwa kushadidisha mivutano na mikwaruzano baina ya Marekani na China.

Serikali ya Beijing imekuwa ikisisitiza kuwa kisiwa cha Taiwan ni sehemu ya ardhi kuu ya China. China imeshaionya Marekani mara kadhaa kwamba haitakuwa tayari kufanya maridhiano yoyote juu ya suala la Taiwan na itatoa jibu kali kwa chokochoko zozote zitakazofanywa juu ya suala hilo.