Russia: Hatuna nia ya kuzikatia gesi kikamilifu nchi za Ulaya
Msemaji wa Ikulu ya Russia (Kremlin) amesema kuwa, Moscow haina nia ya kuzikatia kikamilifu gesi yake nchi za Ulaya.
Matamshi hayo ya Dmitry Peskov yamekuja katika hali ambayo, kwenye kipindi cha miezi ya hivi karibuni, gharama za maisha zimepanda mno barani Ulaya kutokana na mgogoro wa nishati uliosababishwa na vikwazo ambavyo nchi hizo zimeiwekea Russia.
Peskov alisema hayo jana Jumatatu kujibu madai yaliyotolewa na Ursula von der Leyen, Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya aliyedai kuwa, nchi za Ulaya zinapaswa kujiandaa kwa hali mbaya zaidi iwapo Russia itazikatia kikamilifu gesi yake. Hata hivyo Msemaji wa Ikulu ya Russia amesema, Moscow haina nia kabisa ya kufanya kitu kama hicho.

Amesema, Russia haioni shida kuzidhaminia nchi za Ulaya mahitaji yao ya gesi na kwamba tofauti ya inavyodhani Kamisheni ya Ulaya na nchi za Ulaya na Marekani; tangu zamani Russia ilikuwa inadhamini mahitaji hayo muhimu ya nchi za Ulaya, hivi sasa pia inadhamini na katika siku za usoni pia itaendelea kuzipa nchi hizo gesi yake.
Pamoja na hayo Dmitry Peskov amezionya nchi za Ulaya kwa kuziambia kuwa, zisiendelee zenyewe kujitia katika matatizo na baadaye kuzilaumu nchi nyingine kwa matatizo ambayo zimejiingiza zenyewe.
Nchi za Ulaya na Marekani zimeiwekea vikwazo vingi sana Russia kwa madai ya vita vya Ukraine, lakini vikwazo hivyo vimewasababishia matatizo mengi wananchi wa nchi hizo za Magharibi.