Aug 17, 2022 02:37 UTC
  • Trump: Kuondoka Afghanistan lilikuwa tukio la udhalilishwaji mkubwa zaidi katika historia ya Marekani

Aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump amesema, kuondoka majeshi ya nchi hiyo Afghanistan ilikuwa hatua ya pupa na ya udhalilishwaji.

Itakumbukwa kuwa Agosti 15, 2021 kundi la Taliban lilirudi tena madarakani nchini Afghanistan.

Mchakato wa kuondolewa wanajeshi wa Marekani na waitifaki wake nchini humo ulianza Februari 2020, yaani baada ya kusainiwa mapatano kati ya nchi hiyo na kundi la Taliban.

Trump ameeleza kwamba, Marekani ilidhalilika kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa kutokana na uamuzi wa pupa na usio na mpangilio uliochukuliwa na mfuatizi wake Joe Biden kwa ajili ya kuondoka nchi hiyo kijeshi Afghanistan.

Katika taarifa aliyotoa kwa mnasaba wa kutimia mwaka mmoja tangu Washington ilipoyaondoa majeshi yake Afghanistan, rais huyo wa zamani wa Marekani amesema, baada ya Biden kutoa amri ya kundoka Afghanistan, jeshi la Marekani liliacha katika nchi hiyo miongoni mwa silaha bora zaidi duniani zenye thamani ya dola milioni 85.

Kulingana na kauli ya Trump, janga lililozuka mwaka mmoja nyuma nchini Afghanistan lilikuwa tukio la kuaibisha zaidi na la udhalilishwaji mkubwa zaidi katika historia ya Marekani.

Wanajeshi wa Marekani walipoanza kuhamishwa Afghanistan kwa amri ya Trump

 

Pamoja na hayo, Trump ameongezea kwa kusema: "bila shaka sizungumzii suala lenyewe la kuondoa askari, kwa sababu mimi ndiye niliyepunguza idadi ya askari waliokuwepo huko hadi elfu mbili na kuandaa mipango ya kuondoka; ninachozungumzia ni namna ya uondokaji."

Mnamo mwaka 2001, na kwa kisingizio cha kutoa jibu kwa mashambulio yaliyofanywa Septemba 11 mwaka huohuo wa 2001 ndani ya Marekani, serikali ya Washington na waitifaki wake katika shirika la kijeshi la NATO ziliishambulia na kuikalia kijeshi Afghanistan, uvamizi na ukaliaji ardhi kwa mabavu ambao, uliendelea kwa muda wa miongo miwili, kabla ya kuhitimishwa kwa aibu na madhila Agosti 15, 2021.../

Tags