Jun 10, 2016 04:03 UTC
  • Muhammad Ali kuzikwa leo, rais wa Uturuki na mfalme wa Jordan kutohutubia

Nguli wa masumbwi duniani marehemu Muhammad Ali anatazamiwa kuzikwa leo Ijumaa katika mji wa Louisville jimbo la Kentucky nchini Marekani.

Watu 15,000 wakiwemo shakhsia mbali mbali wa kimataifa wanatazamiwa kuhudhuria maziko ya nguli huyo wa ndondi.

Hii ni katika hali ambayo, familia ya Muhammad Ali imekataa maombi ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Mfalme Abdullah II wa Jordan kutoa hutuba wakati wa maziko hii leo.

Bob Gunnell, msemaji wa familia ya Muhammad Ali amesema: "Haijalishi wao ni akina nani na wana vyeo gani, lakini ukweli wa mambo ni kuwa, hatuna nafasi yao katika ratiba yetu."

Muhammad Ali alifariki dunia Juni 3 siku ya Ijumaa akiwa na umri wa miaka 74, baada ya kuugua ugonjwa wa kutetemeka kwa muda mrefu. Bingwa huyo wa ndondi raia wa Marekani mwenye asili ya Afrika, alikuwa akijulikana kama Cassius Clay kabla ya kusilimu na kuitwa Muhammad Ali katika miaka ya 1960.

Hossein Jaberi Ansari, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, marehemu Muhammad Ali aliongoza harakati za kutetea usawa wa watu wa rangi zote bila ya ubaguzi.

Tags