Apr 17, 2024 11:11 UTC
  • Rais wa Uturuki: Israel imempiku Hitler kwa kuua watoto 14,000 wasio na hatia Ghaza

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema, Israel tayari imempiku kiongozi wa Wanazi Adolf Hitler kwa kuua zaidi ya watoto 14,000 wasio na hatia katika Ukanda wa Ghaza.

Erdogan ameyasema hayo alipohutubia mkutano wa wabunge wa chama chake cha Uadilifu na Maendeleo (AK) na kubainisha kuwa, kwa uungwaji mkono usio na masharti kutoka Magharibi, Israel inafanya mauaji ya halaiki huko Ghaza na Ukingo wa Magharibi yanayoacha alama za kutia aibu katika historia ya wanadamu.
 
Rais wa Uturuki ameendelea kueleza kwamba, hakuna anayeweza kuhoji jinsi Uturuki inavyoguswa na suala la Palestina, na akaongezea kwa kudai kuwa kadhia ya Palestina imeyapa maisha yake yeye maana mpya.
 
"Mungu akinijalia uhai, nitaendelea kutetea mapambano ya Palestina, na nitakuwa sauti ya watu wanaodhulumiwa wa Palestina," amesema Erdogan.
Erdogan

Akilinganisha mapambano ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestia HAMAS dhidi ya Israel na Vita vya Kupigania Uhuru vya Uturuki vya zaidi ya miaka 100 iliyopita, Erdogan ameongezea kwa kusema: "Tunafahamu vyema kwamba kuna gharama ya kulipa kwa kutamka haya".

 
Licha ya Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki kusikika mara kadhaa majukwaani akitoa hotuba kali za kulaani jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ghaza, lakini serikali yake imekuwa ikilaumiwa na kukosolewa vikali ndani na nje ya nchi kwa kuendelea kuwa na ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na utawala huo, ambao inaaminika kuwa unaisaidia sana kuendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ghaza, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.../

 

Tags