Rais wa Nicaragua: Kanisa Katoliki ni mfano hai wa udikteta
(last modified Fri, 30 Sep 2022 01:04:00 GMT )
Sep 30, 2022 01:04 UTC
  • Rais wa Nicaragua: Kanisa Katoliki ni mfano hai wa udikteta

Rais wa Nicaragua, Daniel Ortega amelishambulia vikali Kanisa Katoliki na kuitaja taasisi hiyo kuwa mfano hai wa udikteta halisi duniani.

Ortega amesema hayo katika hotuba yake kwa mnasaba wa kuadhimisha miaka 43 tangu kuundwa jeshi la polisi la nchi hiyo na kuongeza kuwa, Kanisa Katoliki linaendeshwa kidikteta kwa kuwa wafuasi wake hawaruhusiwi kuchagua Papa na viongozi wengine wa ngazi za juu wa kanisa hilo.

Rais Ortega ameeleza kuwa, kama kweli kanisa hilo linaheshimu demokrasia, basi lianze kwa kuruhusu Wakatoliki wapige kura kuchagua Papa, makadinali na maaskofu.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Daniel Ortega wa Nicaragua amewataja maaskofu na mapadri wa Kanisa Katoliki kama wauaji na wapangaji wa mapinduzi dhidi ya serikali.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis

 

Kanisa Katoliki nchini Nicaragua limekuwa chini ya mashinikizo ya serikali tokea mwaka 2018, baada ya kutuhumiwa na Ortega kuwa lilichochea maandamano dhidi ya utawala wake. Mamia ya watu waliuawa katika maandamano hayo.

Mwezi Machi mwaka huu, serikali ya Managua ilimfukuza Balozi wa Vatican (Makao Makuu ya Kanisa Katoliki) nchini humo, huku Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis akitoa mwito wa kufanyika mazungumzo baina ya kanisa hilo na Nicaragua.